The House of Favourite Newspapers

Walimu Dar tumieni fursa ya usafiri

0

1

Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva Tanzania (TADWU), Shaban Mdemu akitoa taarifa yake kwa wanahabari (hawapo pichani).

2Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva na Makondakta wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Pazi, (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva Tanzania, Shaban Mdemu.

3Wanahabari wakichukua tukio hilo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari,

Hivi karibuni wamiliki wa vyombo vya usafiri kupitia umoja wao wa (DARCOBOA na UWADA) walifikia muafaka wa kutoa huduma ya usafiri bure kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika Mkoa wa Dar es salaam ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuinua sekta ya elimu. Hatua hii ilikuja baada ya kupokea ombi la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mheshimiwa Paul Makonda, kuwaomba wamiliki hao kuangalia namna ya kuwapunguzia adha ya usafiri walimu ikiwa kama mchango wao katika sekta ya elimu.

Hatua hii ilipokelewa na wadau wa elimu katika mitazamo tofauti huku asilimia kubwa wakilipokea kwa mtazamo chanya na kuona kwamba jamii inaanza kuona thamani ya mwalimu na mchango katika maendeleo ya taifa letu. Hata hivyo wapo baadhi ya watu ambao kwa makusudi wameamua kupotosha dhana hii na kujenga hofu miongoni mwa walimu kwamba upo uwezekano wa walimu kuzalilishwa na madereva na makondakta wa mabasi ya abiria.

Kwa upande wetu madereva na makondakta, tukiwa kama wadau wakuu katika utekelezaji wa programu hii, tumeshtushwa na mtazamo ulijengeka kwa jamii dhidi yetu. Baadhi yao wanatuchora kama watu ambao ni wanyanyasaji, wazalilishaji na watu ambao hatuthamini sekta ya elimu na umuhimu wa walimu kwa jamii na taifa letu. Kauli hizi zimetukera, zimetuhudhunisha na kutudhalilisha kiasi cha kutosha na kamwe hatuwezi kuvumilia kuona kwamba baadhi ya watu wanashusha heshima yetu mbele ya macho ya watanzania kwa maslahi yao binafsi.

Tunapenda watanzania wafahamu kwamba, Makondakta na Madereva tunatambua umuhimu wa walimu kwa ustawi wa nchi yetu. Tunatambua kwamba, bila mwalimu hakuna taifa kwa maana kila raia mwema wa nchi yetu ambaye anatambua wajibu wake na anatoa mchango wake kwa jamii amefundishwa na mwalimu. Tuna ufahamu wa kutosha kwamba, katika historia ya Tanzania walimu wamekuwa na mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Ukombozi wa taifa letu ulipiganiwa na Mwalimu na hata watoto wa makondakta na madereva wanalelewa na walimu. Hivyo, tutakuwa watu wa mwisho katika taifa hili kuwadhalilisha na kuwadarau walimu. Daima tutawapenda, tutawathamini na kuwaona kwamba wao ni nguzo na mhimiri wa Tanzania yetu.

Ndugu wana habari,

Kama Waajiri wetu ambao ni wamiliki wa vyombo vya usafiri walivyolipokea jambo hili na kulipa uzito unaostahiki, vivyo hivyo kwetu Madereva na Makondakta wa mabasi tumeuopokea uamuzi huu kwa namna ya kipekee na tuko tayari kuusimamia na kuutekeleza kwa viwango vinavyotakiwa, kwani tunatambua kwamba jukumu la kuboresha sekta ya elimu inategemea mchango wa kila mtanzania popote alipo na kwa nafasi yake.

Tunatoa wito kwa walimu wote wa Mkoa wa Dar es salaam kuitumia fursa hii waliyoipata bila hofu ili waendelee kutimiza wajibu wao wa kuandaa kizazi bora chenye fikra pevu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, tunatoa wito kwa madereva na makondakta wote Mkoa wa Dar es salaam kuudhihirishia umma wa watanzania kwamba tunatambua kwamba bila walimu tusingeweza hata kutoa na kujumlisha pindi tunapoendesha shughuli zetu, na kwamba tuko tayari wakati wote kuunga mkono juhudi za kuwainua walimu nchini. Tunaisubiri siku ya kesho kwa shauku kubwa, ili nasi tuanze kutoa mchango wetu kwa walimu. Walimu msihofu, madereva na makondakta tuko nyuma yenu.

Vilevile tunawaomba wadau wengine wajitokeze kuiga mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makonda na Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri ili kuwapa motisha walimu wetu ambao ndiyo walezi wa watoto wetu.

Tunaamini kwamba, mchango huu unaotolewa na wadau wa sekta ya usafiri umefungua njia ya mjadala mpana zaidi kuhusu mazingira ya walimu wetu na jitihada zinazopaswa kuchukuliwa ili kuwajengea mazingira rafiki ya kutoa elimu bora kwa watoto wetu.

ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA

IMETOLEWA NA;

Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva Tanzania (TADWU), Shaban Mdemu

(HABARI/PICHA: DENIS MTIMA/GPL)

Leave A Reply