Waliokufa ajali ya moto Moro… UTATA WAIBUKA!

 

WAKATI tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikisubiriwa kutoa majibu ya kuwepo au kutokuwepo kwa uzembe kwa mamlaka husika za serikali juu ya ajali ya moto iliyoua watu 89 mpaka sasa mkoani Morogoro, utata umeibuka, Uwazi limebaini.

 

Hivi karibuni lori la mafuta lililipuka katika Kijiji cha Itigi, eneo la Msamvu na kusababisha vifo hivyo na majeruhi zaidi ya mia. Ingawa sababu za kulipuka kwa lori hilo hazijawekwa wazi lakini tukio hilo limetajwa kusababishwa na harakati za watu waliokwenda kufungua vizibo vya tanki la mafuta kwenye gari hilo kwa lengo la kujipatia bidhaa hiyo kinyume cha sheria.

 

DONDOO ZA UTATA

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali na uchunguzi wetu mambo kadhaa yameibua utata yakiwemo baadhi ya ndugu kupotelewa na jamaa zao mpaka leo hawajulikani walipo.

 

Aidha imedaiwa kuwa miongoni mwa watu waliokufa hawakuwepo eneo la tukio kama inavyodaiwa kuwa waliodhurika wengi walikuwa wamekusanyika kuteka mafuta kutoka kwenye lori hilo. Nao baadhi ya watu wameibuka na madai kwamba, mmiliki wa gari lililolipuka awalipe fidia wale ambao wamejeruhiwa na kupoteza maisha.

 

UTATA WALIOKUFA..

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Uwazi baadhi ya ndugu waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo mbaya wamesema licha ya ndugu zao kudaiwa kufa kwenye tukio hilo lakini walisema hawakuwa miongoni mwa watu waliokwenda eneo la tukio kujipachotea mafuta.

 

“Nina siku ya tatu sijamuona mwanangu, simu yake haipatikani, rafiki zake wananiambia huenda amekufa kwenye ajali hiyo. “Nimewauliza amekufa kwani naye alikwenda kuiba mafuta, wakasema moto ulisambaa ovyo na kuwaunguza hata waliokuwa kando ya eneo la ajali,” alisema Mzee Ally Masoud mkazi wa Msamvu.

 

Naye kijana Rashid Said ambaye ni dereva wa bodaboda mjini Morogoro alisema: “Mimi nilikuwa kando naangalia tukio, kama nisingewasha pikipiki na kuondoka haraka nami ningepoteza maisha maana moto ulikuwa unasambaa kwa kasi kubwa.”

MAFUTA YALIVYOTAPAKAA

Mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo ambaye anajinasibu kwamba awali alifanikiwa kuchukua video ya tukio kuonesha watu walivyokuwa wakigombania kuteka mafuta kutoka kwenye lori hilo alisema: “Yaani baada ya koki za tanki kufunguliwa na baadhi ya vijana, mafuta yalianza kumwagika na kutengeneza kama mto kuelekea sehemu mbalimbali.

 

“Watu wakati wanateka wakawa kama wanaogelea kwenye madimbwi ya mafuta, baada ya muda eneo lote likawa na unyevunyevu wa mafuta ya petroli. “Harufu ikaenea kote, nilipoona hivyo ikabidi niondoke kwa sababu nilikuwa nawahi kwenye kazi zangu, sijafika mbali ndiyo nikasikia mlipuko huo umetokea.”

 

MAMAN’TILIE AFUNGUKA

“Hapa siyo porini ni mjini, shughuli za kila siku zinaendelea, ndiyo maana kuna mabanda ya vyakula na wafanyabishara ndogondogo. “Kuna mwenzetu kalazwa kwa sababu alivamiwa na moto kwenye banda lake, hawa vijana wa bodaboda ambao ndiyo waliokuwa wengi walikuwa wakiteka mafuta wanapita mitaani kwenda kuyaficha wanakojua.

 

“Lakini kwa sababu nguo na nyayo zao zilikuwa zimenasa mafuta ni kama walikuwa wakiyasambaza, ndiyo maana umeona eneo lote limewaka moto na kuwakumba hata wasiohusika,” alisema Stella John.

 

WATAKA FIDIA

Baadhi ya watu kutoka eneo la tukio walisema ipo haja ya majeruhi na waliopoteza maisha bila kuwa sehemu ya ajali hiyo kulipwa fidia na mmiliki wa lori hilo kama haki yao ya msingi. “Serikali ifanye uchunguzi wake, itabaini kuna watu hawakwenda kwenye ajali, wamevamiwa na moto kwenye maeneo yao ya biashara bila kujua kwa sababu petroli ilisambaa eneo kubwa.

 

“Sasa kwa kuwa magari yana bima za ajali, asilipwe mwenye gari tu na hawa ambao hawahusiki na chanzo cha moto lakini wamepata madhara walipwe,” alisema Fredy Macha ambaye alijitambulisha kuwa ni mfanyabiashara eneo la Stendi Kuu ya Mabasi ya Msamvu.

MISIBA YATENGWA, YAONDOLEWA

Wakati mwandishi wetu akifanya uchunguzi katika tukio hili alibaini kuna baadhi ya familia ambazo zimekuwa kwenye utata mkubwa wa aidha kuweka msiba au kutoweka.

 

Akizungumza na Uwazi, Joseph Damas, mkazi wa Mtaa wa Mwanzo Mwisho, Kata ya Mwembesongo alisema: “Hata sijui cha kufanya, kuna wakati tunaweka msiba halafu baadaye tunaambiwa kijana yuko hai, lakini hatufahamu mpaka sasa yuko wapi maana ametoweka nyumbani toka siku ya tukio.”

 

Adha, familia nyingine ambayo imekuwa katika utata wa kutojua la kufanya ni ya Mzee Abdul wa eneo la Mafisa ambaye amesema: “Nimekwenda hospitali kijana wangu hayupo, nimejitokeza kuangalia waliokufa nako vipimo bado havijamtambua.”

 

TUJIKUMBUSHE

Agosti 10, lori la mafuta lilipinduka eneo la Msamvu ambapo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wengi wakiwemo waendesha pikipiki walijitokeza kuchota mafuta baada ya koki za tanki kufunguliwa na wasiojulikana.

Hata hivyo, baadaye wakati baadhi ya wananchi wakiendelea kuchota mafuta hayo kutoka kwenye lori hilo mlipuko wa moto ulitokea na kujeruhi watu kadhaa huku wengine takriban 70 wakipoteza maisha kwa kuunguzwa vibaya. Gazeti hili linatoa pole kwa wote walioguswa na misiba hiyo na linawaombea majeruhi wapone haraka.


Loading...

Toa comment