The House of Favourite Newspapers

Wanadiplomasia Kushirikiana na Tanzania Kuvutia Wawekezaji

0
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akieleza jambo kwa Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchin, Manfred Fanti, wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji leo Januari 22,2021 Jijini Dodoma.

UMOJA wa Ulaya (EU) umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kuja kuwekeza hapa nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akisisitiza jambo kwa Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Bibi Lianne Houben, ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini Uholanzi.

Hayo yamesemwa leo, Januari 22, 2021 jijini Dodoma na Manfred Fanti, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

 

“Nimekuwa nikisikia ushuhuda kutoka kwa wawekezaji wengi wanaotoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwa wanapata faida katika uwekezaji wao hapa nchini na nikiwa kama mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania ni jukumu langu kuhakikisha kuwa nashirikiana ipasavyo na Serikali ya Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza Tanzania,” alisema Fanti.

 

…Mkumbo (kushoto) akipokea kitabu kinachoeleza masuala mbalimbali kuhusu nchi ya Uholanzi kutoka kwa Houben mara baada ya mazungumzo yao leo jijini Dodoma kuhusu masuala ya uwekezaji.

 

Aliongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unatambua jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli katika kuboresha mifumo ya kisheria, kisera na ya kitaasisi ili kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayovutia wawekezaji na hivyo wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kufanikisha lengo hilo.

 

 

 

Katika mazungumzo hayo Mkumbo na Fanti walijadili pia maeneo bayana  ambayo Tanzania na Umoja wa Ulaya wanaweza kukuza ushirikiano wa uwekezaji  ikiwemo katika sekta ya uzalishaji nguo, uchimbaji na uchakataji wa madini, uchakataji wa mazao ya mifugo na uvuvi, uzalishaji wa nishati.

Mkumbo akiwa na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Manfred Fanti mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji leo Dodoma.

Pia  Mkumbo aligusia baadhi ya maeneo ya kimkakati ambayo tayari serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka nguvu kuyatekeleza ikiwemo kuandaa na kutekeleza  Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji, utekelezaji wa programu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara (ROADMAP) pamoja na kuandaa mfumo kabambe wa ukusanyaji takwimu za uwekezaji nchini.

 

Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa hayo ni baadhi ya maeneo ambayo Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya, ili pamoja na mambo mengine, kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni hapa nchini.

 

Kwa upande mwingine eaziri huyo wa alikutana pia na Houben, Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hususani wanaotoka nchi ya Uholanzi.

 

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kuziwezesha Taasisi mbalimbali Wezeshi zinazohudhumia wawekezaji kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku zikizingatia maslahi mapana ya wawekezaji, pamoja na suala la uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na fani mbalimbali ambazo wawekezaji wanazihitaji.

 

Uholanzi ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi nchini Tanzania waliowekeza katika sekta za mbalimbali kama vile kilimo (kwa mfano makampuni ya maua yaliyowekeza mikoa ya Arusha na Kilimanjaro), huduma za kifedha (kwa mfano Benki ya NMB), Viwanda (kwa mfano Kampuni Unilever na Heineken), usafirishaji (kwa mfano Kampuni ya KLM).

 

Takwimu zinaonyesha kuwa takribani miradi 161 ya kutoka Uholanzi  imesajiliwa katika za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na mitaji yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani biilioni 1.1 na kutoa ajira 13,995.

Leave A Reply