The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Majeruhi Ajali ya Arusha… Maombi Yamejibu

0
Doreen akiwa na mzazi

 

SIKU 46 tangu wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya jijini Arusha wafike nchini Marekani kwa ajili ya matibabu kufuatia ajali ya gari iliyotokea Mei 6, mwaka huu na kuwaua wenzao 32, wametoa faraja kitu kinachoonyesha maombi yamejibu.

Watoto hao watatu, Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Sadya Awadh walipelekwa Marekani kwa msaada wa ndege ya Shirika la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa Muhubiri maarufu duniani, Bill Graham.

 

Shadia

 

Vijana hao ambao wamekuwa wakipata matibabu na kuimarika afya zao kwa kasi, wanatibiwa katika Hospitali ya Mercy iliyopo jijini Sioux katika Jimbo la Iowa, ambayo ni miongoni mwa hospitali 30 bora nchini Marekani.

Kwa mujibu wa mwalimu mmoja wa shule hiyo ya Arusha, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa kile alichosema wamezuiwa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya suala hilo, watoto hao wametoa salam za kuwashukuru Watanzania kwa kuwaombea, kwani wanaendelea vizuri na matibabu.

 

Wilson

 

“Kwa kweli wanaendelea vizuri sana, ingawa taarifa nyingi tunazipata kupitia mitandao, lakini walipozungumza kwa mara ya mwisho na uongozi, walitoa shukurani hizo. Na hapa shuleni, wanafunzi wenzao wanawaombea kwa sala ili warejee nyumbani kuungana nao kwenye masomo,” alisema mwalimu huyo.

Watoto hao ambao waliondoka nchini wakiwa hoi, hivi sasa wanaendelea kupata nafuu kiasi cha kuanza kufanyishwa mazoezi ya kutembea, kucheza mpira na hata kufanya matembezi mafupi kwa ajili ya kuburudisha akili.

“Wanafunzi wenzao huku nao hivi sasa wameanza kuzoea maisha baada ya ajali ile mbaya, walitafutiwa wanasaikolojia ambao walikuja hapa kuwaweka sawa. Kila mmoja ana hamu kubwa ya kuwaona wenzao hao wanarejea wakiwa wamepona,” alisema.

Taarifa nyingi za watoto hao zimekuwa zikitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini ambaye amekuwa kiungo muhimu kati ya wahisani hao waliojitokeza kuwasaidia watoto hao waliopata majeraha mabaya.

Siku walivyosafirishwa kwenda kutibiwa Marekani.

Basi la shule hiyo ya Lucky Vincent, wakati likielekea Karatu kwa ajili ya ziara ya kimasomo, liliacha njia na kuingia korongoni Mei 6, mwaka huu na kuua watu 35 papo hapo, wakiwemo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

 

Eneo la Ajali ya Wanafunzi wa Lucky Vincent, Karatu

Leave A Reply