The House of Favourite Newspapers

Afukuzwa Kijijini Akituhumiwa Kuwaingilia Wanawake Kishirikina

0

WANANCHI wa Kitongoji cha Ikonda bondeni Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe wamemfukuza mkazi aliyehamia katika kitongoji hicho akitokea kijiji cha Ilevelo, Mateso Mbilinyi, wakimtuhumu kuwaingilia kimwili kwa njia ya ushirikina baadhi ya wanawake wa kitongoji hicho.

 

Katika mkutano wa kitongoji hicho uliofanyika kwenye kitongoji hicho wananchi wameelekezea tuhuma kwa Mateso wakisema amekuwa akiwaingilia kimwili kwa njia za ushirikina huku akipita mtaani na kujisifia kwa vitendo hivyo.

 

Kaimu Afisa Mtendaji kata ya Tandala, Robert Nko, kwenye mkutano huo alianza kuhoji uhalali wa mtuhumiwa kuishi katika kijiji cha Ikonda kama alifika na barua ya utambulisho kutoka kijiji cha Ilevelo.Wananchi walidai mtuhumiwa huyo anafanya vitendo hivyo na kutamba mitaani, hivyo wakataka arudishwe alikotoka la sivyo watamchukulia hatua za kisheria.

 

Naye Mateso  alisema  tuhumu dhidi yake si za kweli na kwa kuwa alishatuhumiwa katika kijiji alichotoka cha Ilevelo, kwa tuhuma kama hizohizo, amesema hata hizo zilizoelekezwa dhidi yake ni kwa kuwa jina lake limechafuliwa toka mwanzo kwamba yeye ni mshirikina.

 

Amesema pamoja na hayo yupo tayari kutii maagizo ya wananchi hao wanaomtaka aondoke kijijini hapo.Katika mkutano huo Balozi wa eneo lake ametolea ufafanuzi utata uliojitokeza kuhusu barua ya utambulisho aliyokuja nayo mtuhumiwa katika kijiji cha Ikonda akitokea Ilevelo akisema alikuwa amekuja hapo kwa ajili ya matibabu.

 

Naye Nko alisema serikali watatii maagizo ya wananchi kwa kumwandikia barua ya kuondoka kijijini hapo kwenda alikotoka na watafuata taratibu zote za serikali ili kumfikisha salama kijijini hapo.

 

Kitongoji cha Ikonda-Bondeni kipo karibu na hospitali kubwa ya Ikonda inayomilikiwa na taasisi ya kidini, na ikiwa maarufu kutokana huduma zinazotolewa na kusababisha wageni wengi kutoka nje ya wilaya na mkoa kufika kwa ajili ya matibabu.

Leave A Reply