The House of Favourite Newspapers

Wanaoiua Yanga Hawa Hapa

0

YANGA imetoka sare ya 0-0 dhidi ya Coastal Union na kuandika sare yake ya nane kati ya mechi 22 za Ligi Kuu Bara ilizocheza! Yanga imebaki nafasi ya nne ikifikisha pointi 41 na bado Namungo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43 lakini kinachoonekana kuwa wingi wa wachezaji wengi wa kimataifa wasio na msaada ndio wanaoiua Yanga.

 

 

Licha ya kuwa na wachezaji tisa wa kimataifa, katika mechi ya Jumapili iliyopita, Yanga imewatumia wachezaji watatu tu wa kimataifa ambao ni Bernard Morrison raia wa Ghana, Papy Tshishimbi (DR Congo), Haruna Niyonzima (Rwanda) na Lamine Moro, Ghana pia.

 

Lakini kuna wachezaji wa kimataifa kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga ambao kutokana na kutokuwa na mchango wowote na sasa hawatumiki.

 

Wachezaji hao ni mshambuliaji David Molinga kutoka DR Congo, Yikpe Gnamien raia wa Ivory Coast, Erick Kabamba (Zambia) na Papy Sibomana kutoka Rwanda ambao Kocha Luc Eymael anaonekana wazi kutokubaliana na viwango vyao hivyo kuwaacha jukwaani kabisa.

 

“Kwa kweli kuna tatizo kubwa katika suala la ushambuliaji, humu ndani wote tunaelewa na wakati mwingine badala ya kulaumiana tunaona bora kupambana kwanza, tutalaumiana mwishoni. Lakini wachezaji wengi wa nje hawana nafasi, hawana msaada na wakati mwingine wamekuwa si chaguo la kocha kwa kuwa hawakubali,” kilieleza chanzo kutoka ndani ya Yanga.

 

Yikpe alisajiliwa kwa mbwembwe sana, lakini ameshindwa kuwa msaada pamoja na kufunga bao moja hali ambayo imesababisha mashabiki kumzomea mara kadhaa huku Molinga naye akishindwa kufanya kazi yake kama wengi walivyotarajia.

 

Jambo hili ndilo linaonekana kuiua Yanga kutokana na kutokuwa na nguvu kubwa katika ushambulizi na hasa kufunga mabao, hali inayoifanya timu hiyo kuendelea kusuasua na kusababisha iambulie sare nne mfululizo.

Sare nne maana yake Yanga imepoteza pointi nane katika mechi nne mfululizo, jambo ambalo linathibitisha kuwa wazi sasa wamejiondoa katika mbio za ubingwa.

 

Sare hizo zinaonekana wazi katika mechi za Yanga kwa kuwa inashambuliwa mara nyingi sana na inakuwa na mashambulizi machache sana, hali inayozima matumaini kwa kuwa wachezaji hao wanaolipwa fedha nyingi, hawana msaada kama uliotarajiwa.

 

Idadi hii kubwa ya wachezaji kutoka nje wasiotumika, inaifanya Yanga kuendelea kulipa mishahara yao bila ya kupata kile ambacho wao wanastahili na sasa inaonekana watalazimika kuachana nao baada ya msimu huu au unaweza kusema, hali ilivyo huu si msimu wa Yanga tena.

 

Watani wao Simba wanaongoza ligi wakiwa na pointi 62, hii ni baada ya kucheza mechi 24, sasa tofauti ya mechi mbili tu na Yanga ambao wana pointi 41, maana yake tofauti ya pointi 21 na kama wakishinda michezo yao ya kiporo, tofauti itakuwa pointi 15, hali inayoonyesha wazi haitakuwa rahisi kuikamata tena Simba.

Leave A Reply