The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Wanariadha Waagwa, Waahidi Kurudi na Medali

0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harisson Mwakyembe.

 

TIMU ya taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya riadha ya dunia yanayoanza wiki hii jijini London, Uingereza,  leo imeagwa jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa rasmi bendera ya taifa wakiwa wawakilishi maalum wa Tanzania katika mashindano hayo makubwa.

 

Timu hiyo yenye wanariadha wanane imeagwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harisson Mwakyembe,  na kuhudhuriwa na maofisa mbalimbali akiwemo Rais wa Chama cha Riadha Tanzania,  Anthony Mtaka na Mkurugenzi Mtendaji wa Multi choice Tanzania, Maharage Chande, ambao ni wadhamini wakuu wa timu hiyo.

 

Rais wa Chama cha Riadha Tanzania, Anthony Mtaka.

 

Akizungumza katika hafla hiyo,  Mwakyembe amesema wizara yake iko bega kwa bega na wadau wa michezo hapa nchini katika kuhakikisha  nchi inapiga hatua katika sekta hiyo na kuifanya moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa wanamichezo nchini.

Amesema serikali imejidhatiti kikamilifu  kuratibu na kurasimisha michezo nchini ili wanamichezo watambue kuwa hiyo ni kazi ya heshima na yenye malipo makubwa.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Multi choice Tanzania, Maharage Chande.

 

 

“Kwanza kabisa nimetiwa moyo sana na ari ya vijana waliyo nayo na kama mlivyoona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, vijana hawa wamepikwa vizuri na wana ari, moyo na uzalendo mkubwa na kilicho mbele yao ni kitu kimoja tu, kupambana kufa na kupona na kurudi na medali,” alisema.

 

Mwanariadha Alphonce Simbu akizungumza na wanahabari.

 

Waziri pia ameipongeza kampuni ya Multi choice Tanzania kwa udhamini wake mkubwa katika maandalizi ya timu hiyo ambapo kampuni hiyo ilikuwa mdau mkubwa katika kufanikisha mafunzo katika kambi hiyo.

Naye Mtaka amesema mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na chama hicho bado zipo changamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu za pamoja ili kuhakikisha riadha inaendelela.

 

Mwakyembe akikabidhi bendera.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Multi Choice Tanzania, Maharage Chande,  amesema kampuni yao ina dhamira endelevu ya kuibua na kuendeleza vipaji  nchini na ndiyo sababu wakaamua kusadia katika maandalizi ya timu hiyo.

 

NA DENIS MTIMA | GLOBAL PUBLISHERS

Leave A Reply