The House of Favourite Newspapers

Wanaume Tandale watoboa siri za ‘mafataki’

0
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwa Tumbo, Hatibu Kibwama akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Mtandao wa Ushiriki wa Wanaume Tanzania (MenEngage Tanzana – MET) kwa lengo la kujadili nafasi ya mwanaume na wajibu wake katika kutokomeza mimba za utotoni.

KUFUATIA ongezeko la mimba za utotoni pamoja na ukatili wa kingono katika kata ya Tandale jijini Dar es Salaam, baadhi ya wanaume katika kata hiyo wamesema mojawapo ya sababu zinazochangia kukithiri kwa vitendo hivyo ni ukosefu wa shule za sekondari.

 

Pia  ukosefu wa huduma rafiki za afya ya uzazi, umasikini, kutokuwepo kwa usawa wa kijinsi kati ya mtoto wa kike na wa kiume kuanzia ngazi ya jamii, mila na tamaduni hatari, uelewa finyu miongoni mwa wanajamii juu ya madhara yatokanayo na vitendo hivyo ni baadhi ya sababu zilizotajwa na wanaume hao.

Mratibu wa Mtandao wa MET, Yared Bagambilana, akizungumza katika mdahalo ili kuchagiza utekeleza wa mpango mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwa).

 

Hayo yamebainishwa juzi jijini Dar es Salaam katika mdahalo maalumu uliofanyika katika kijiwe cha kahawa kilichopo Kata ya Tandale kwa Tumbo.

 

Mdahalo huo ulioandaliwa na Mtandao wa Ushiriki wa Wanaume Tanzania (MenEngage Tanzana – MET) chini ya uratibu wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), ulilenga kujadili nafasi ya mwanaume na wajibu wake katika kutokomeza mimba za utotoni.

 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwa Tumbo, Hatibu Kibwama alisema katika kata hiyo ya Tandale hakuna shule yake ya Sekondari jambo linalowalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu na kukutana na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.

 

Mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Kwatumbo, Tandale akizungumza sababu za ongezeko la mimba za utotoni pamoja na ukatili wa kingono katika kata hiyo.

 

“Kwa sababu baadhi yao wanasoma kule Kibamba au huko Gongolamboto, kwa umbali huu ni lazima mazingira yawe hatarishi kwa watoto wa kike. Tuna kesi za mimba za utotoni ambazo zimeripotiwa na nyingine hazijaripotiwa na wazazi.”

 

Hoja hiyo iliungwa mkono na Sauda Mtale ambaye alisema mazingira watoto wa kike kupata mimba kwa sababu mazingira wanayoishi ni magumu.

“Hawapati mahitaji muhimu kujikimu, lakini pia baadhi yao hawalelewi na wazazi wao, wanajitegemea.”

 

Aidha, mmoja wa wakazi wa mtaa huyo Adam Khalifan alisema; “Kuna kauli zinasema, mtoto wa mwenzako ni wako, lakini wanaume wengi wana kauli mpya sasa kuwa mtoto wa mwenzio ni mkubwa mwenzio. Ndio maana mimba za utotoni zinaongezeka.”

 

Ally Mtamiro alisema “Asilimia kubwa katika familia zetu hatuna muda wa kukaa pamoja na kujadili kuhusu afya na jinsi gani watoto wa kike wanaweza kujikinga na mimba za utotoni. Pia mazingira yanatubomoa, kila nyumba watoto wamepata ujazuito, hivyo historia inajirudia.”

 

Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto, Manisapaa ya Kinondoni, Clara Urasa, alisema “Hata Tandale mimba za utotoni ni changamoto. Wasichana wapo ambao wamekatiza ndoto zao za kuendelea na elimu kwa sababu ya mimba za utotoni.”

Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto, Manisapaa ya Kinondoni, Clara Urasa, akizungumza katika mdahalo huo

 

Aidha, Mratibu wa Mtandao wa MET, Yared Bagambilana, alisema midahalo ya aina hiyo inalenga kuchagiza utekeleza wa mpango mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake  na Watoto (Mtakuwa).

 

“Tunalenga kuhamasisha kubadili tabia na vitendo vinavyofanywa na wanaume ambavyo huathiri ustawi wa wanawake na watoto na maendeleo ya tafia kwa ujumla katika Nyanja zote za kimaisha.

 

“Kwa sababu tafiti zilizofanywa na Sonke Gender Justice na Instituto Promundo zinaonyesha wanaume wanne kati ya watano ni baba, au wanaelekea kuwa kina baba, walimu, marafiki, wajomba wa watoto, hivyo basi mwanaume ni mtu wa karibu sana wa mtoto na ana wajibu wa kushiriki katika malezi ya mtoto kikamilifu,” alisema.

 

Leave A Reply