The House of Favourite Newspapers

Wanaume Zanzibar Watoa Talaka kwa Njia ya SMS

0

WANAUME visiwani Zanzibar wanadaiwa kutoa talaka kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi (SMs), kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni dharau na kinyume cha mila za Kizanzibari.

 

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, ameeleza kukerwa na kukithiri kwa tabia hiyo na kueleza kuwa ni ukiukwaji wa mila Kizanzibari.

 

Amesema hayo juzi wakati akifunga mafunzo ya ndoa awamu ya tano yaliyotayarishwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mufti Zanzibar.

 

Aliwataka wanandoa watarajiwa kuepuka talaka za kiholela ambazo athari zake ni kubwa katika jamii ikiwamo kutelekezwa kwa familia na watoto kutaabika.

 

‘’Talaka zimekuwa nyingi nyingine zikitolewa kinyume cha utaratibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, huo ni ukiukwaji wa maadili na mila za Kizanzibari,’’ alisema.

 

Mgeni aliipongeza Ofisi ya Mufti wa Zanzibar kwa kuandaa mafunzo kwa wanandoa, ambayo alisema yatasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti talaka za kiholela. Alisema utoaji wa talaka kiholela kwa kiasi kikubwa unadhihirisha kwamba watu wanaingia katika ndoa bila ya kupata elimu juu ya ndoa na familia.

 

‘’Nimefurahishwa na utaratibu wa mafunzo kwa wanandoa watarajiwa, hii ni mara ya tano hivi sasa utaratibu huu kufanyika ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza talaka,’’ alisema.

 

Mshauri wa Ofisi ya Mufti, Shehe Fadhil Soraga, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu wanandoa watarajiwa kufahamu majukumu yao ili kuzifanya ndoa zao kuwa endelevu.

 

‘’Huu ni muhula wa tano wa mafunzo kwa wanandoa watarajiwa, ambapo lengo ni kuzifanya ndoa kuwa endelevu na kuepuka talaka ambazo athari zake ni kubwa ikiwamo kutelekezwa kwa watoto,’’ alisema.

 

Ali Juma (23) ambaye anatarajiwa kufunga ndoa mapema mwakani aliyeshiriki mafunzo hayo, alisema yamemsaidia kuzifahamu haki zinazostahiki katika ndoa yake na jinsi ya kuidumisha. Jumla ya vijana 120 wamehitimu mafunzo hayo awamu ya tano kwa wanandoa watarajiwa ambayo yanaendeshwa na kusimamiwa na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar.

Leave A Reply