The House of Favourite Newspapers

Wanne Mbaroni kwa Kusambaza ‘Uvumi wa Kuugua Rais Magufuli’

0

WATU wanne wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kwa madai ya kusambaza habari za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa rais wa Tanzania John Magufuli anaumwa ikiwa ni kinyume na sheria ya makosa ya kimtandao.

 

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la polisi nchini humo, mtu mmoja alikamatwa mkoani Iringa, mwingine jijini Dar es salaam na wawili wamekamatwa mkoani Kilimanjaro.

 

 

Watu hao wanatuhumiwa kuchapicha katika mitandao ya kijamii ikiwemo mtandao wa facebook taarifa hizo za uzushi kuwa rais Magufuli anaumwa.

 

 

‘’Tutaendelea kuchukua hatua kali sio tu kwa wanaosambaza taarifa za uongo za rais Magufuli bali zozote zitakazobainika ni za uongo’’ amesema kamanda msaidizi wa polisi mkoa wa Iringa Rienda Millanzi.

 

 

Mara ya mwisho kwa rais Magufuli kuonekanaka hadharani ilikuwa Jumamosi ya Februari 27. Hata hivyo mwishoni wa juma lililopita Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa Magufuli yupo na anaendelea na kazi.

 

 

Majaliwa alitahadharisha kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa unaofanyika juu ya afya na alipo rais Magufuli katika siku za hivi karibuni.

 

 

Wakati huo huo makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga amewataka watanzania kuacha kusikiliza maneno ya watu wa nje na kuwa na umoja.

 

 

‘’Nataka niwaambie kwamba wakati muhimu wa watanzania kushikamana ni wakati huu, kujenga umoja ni wakati huu, si wakati wa kusikiliza maneno yanayotoka nje nasi yakatuparaganya vichwa, uimara wa taifa letu unaleta maneno mengi,’’ amesema Makamu wa Rais Samia Suluhu.

Leave A Reply