The House of Favourite Newspapers

Wanne Watiwa Mbaroni kwa Kutaka Kumuibia Rais

0

HII nayo kali! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia jamaa wanne kukamatwa kwa njama ya kujaribu kumuibia Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kipande chake cha ardhi.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi nchini humo, wanne hao walikamatwa wakishukiwa kupanga njama ya kutaka kuuza shamba hilo lililopo katika mtaa wa kifahari wa Karen.

 

Watu hao ambao ni Mohamed Muhammud, James Opere, Jonah Tuuko na Samakin Lesingiran walifikishwa mahakamani jijini Nairobi kwa kesi hiyo na wataendelea kusalia kuzuizini ili kuruhusu polisi kuendelea na uchunguzi.

 

Hakimu anaesikiliza kesi hiyo, Jane Kamau alisema watu hao wanaweza kuachiliwa leo kwa dhamana ya KSh 30, 000 sawa na zaidi ya shilingi laki 4 ya kitanzania kila mmoja.

 

Upande wa mashtaka ulisema kipande hicho cha ardhi kiko katika eneo la Windy Ridge na wanne hao waliingia katika shamba hilo kwa lazima Januari 3 na kutafuta mipaka ya shamba hilo huku afisa anayeendesha uchunguzi akiiambia mahakama kuwa nia yao ni kuliuza.

 

Alisema licha ya kuwa shamba hilo linamilikiwa na Rais Kenyatta, kuna hati miliki feki ambayo watu hao wanaitumia kuwahadaa wanunuzi ambalo ni kosa jingine kisheria.

 

Aliitaka mahakama kumpa muda wa kuendeleza uchunguzi huku wanne hao wakizuiliwa ili afaulu kupata aliye na hati miliki hiyo feki. Taarifa za kisa hicho zimeibua hisia tofauti mtandaoni wengi wakihoji ni vipi walipata nguvu za kujaribu kumuibia rais na hapa ndipo ule msoemo ‘ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni’.

Leave A Reply