The House of Favourite Newspapers

Wanyarwanda wakataa mamilioni ya Yanga SC

KLABU ya Rayon Sports ya Rwanda imekataa dau lililotolewa na Yanga kwa ajili ya kukamilisha usajili wa beki wao, Abdul Rwatubyaye.

 

Yanga walipeleka kitita cha dola 40,000 lakini zimekataliwa na timu hiyo ambayo imesema inataka dola 80,000. Yanga inamtaka beki huyo ikiamini kuwa anaweza kuwasaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa zinasema kuwa baada ya Yanga kupeleka ofa hiyo wamekataliwa na kuelezwa kuwa warudi wakajipange kutafuta dola nyingine 40,000.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, uongozi wa Yanga ulifanya mawasiliano na meneja wa beki huyo na kuweka ofa yao ya dau hilo la fedha kabla ya yeye kuwatajia kiasi wanachotakiwa kukitoa ili wapate saini yake.

 

Mtoa taarifa huyo alisema, Yanga tayari wamepewa taarifa za beki huyo ambayo inatakiwa ivunje mkataba wa miaka miwili alioubakisha Rayon kati ya mitatu aliyoisaini kwenye msimu uliopita.

 

“Usajili wa Rwatubyaye ni kama umekamilika kwa asilimia kadhaa kwa maana ya viongozi wa Rayon, Yanga na meneja wa mchezaji huyo kwenda vizuri, ni baada ya Yanga kupeleka ofa yao ambayo inajadiliwa hivi sasa.

 

“Yanga wameleta dau lao, lakini ni dogo, ni dola 40,000, ukweli utakuwa ngumu kwa kuwa bei ya beki huyo ni dola 80,000, tumewaambia wakajipange upya warudi tena, leo (jana) tulipanga kuzungumza tena,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika hivi karibuni alilithibitishia gazeti hili kuwa wapo kwenye mazungumzo mazuri na beki huyo kwa ajili ya kutua kuichezea timu katika usajili wa dirisha dogo.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.