The House of Favourite Newspapers

Washiriki N.P.S.C Waendelea Kutoa Ushuhuda

0

WAKATI shindano la kusaka vipaji vya vijana wenye uwezo wa kuzungumza mbele ya hadhara likizidi kuchanja mbuga, baadhi ya washiriki wa shindano hilo lililopewa jina la National Public Speaking Competition wameelezea namna walivyofanikiwa kupenya 30 bora.

 

JOSEPH RAYMOND MEENA

Ni mjasiriamali. Taarifa za shindano nilizipata kupitia mitandao ya kijamii (Instagram).

Shindano limekuwa na matokeo mazuri tangu mwanzo kwa sababu limetuwezesha sisi kama vijana kukutana na kufahamiana na watu mbalimbali wa sekta ya uzungumzaji.

 

Pia kupitia mashindano watu wengi tumeweza kutambua uwezo tulionao kama wazungumzaji. Kwa waliojiandaa vizuri na kusikiliza maoni ya majaji wakati wa mashindano waliweza kufanya vizuri na kusonga mbele kwenye hatua zilizofuata.

 

MLEBE SADICK SAID (23)

Ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kuu cha Dar es salaam, nasomea taaluma ya ualimu.

Niliipata taarifa ya mashindano haya Disemba mwaka jana kutoka kwa rafiki yangu Victor Mwambene aliyekuwa ameshachukua fomu pia ya shindano hili.

 

Nilipata ugumu kidogo mwanzoni nilivyoona idadi kubwa ya washiriki wenye uwezo mkubwa nikapata hofu nitapenyaje kwenye mchuano huu ili kufika 30 bora.

Lakini nilijitahidi kufuata ushauri wa majaji kila waliponirekebisha. Matumaini yangu makubwa ni kuongeza maarifa zaidi ya uzungumzaji mbele za watu na kuwa katika historia ya shindano hili.

CHEDIEL RICHARD WAZOEL

Nilipata taarifa ya mashindano haya kupitia kwa baba yangu aliyeona tangazo kupitia Channel 10.

Ndipo alinijulisha nikafuatilia kupitia Instagram nikapata taarifa kamili na Disemba mwaka jana nikaenda kuchukua fomu tena namba moja.

 

Safari kuelekea Top 30 ilikuwa ngumu kwa sababu nilikuwa nashindwa kufikisha ujumbe vizuri kwa hadhira.

Hata hivyo, baada ya kufanya mazoezi nimefanikiwa kuvuka. Matarajio yangu ni kukuza kipaji changu zaidi.

 

ALLY MFAUME

Ni mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Mara ya kwanza tangazo la shindano hili nililiona kwenye akaunti ya Facebook ya Eric Shigongo.

Mchakato mzima haukuwa rahisi kwani watu wengi walikuwa wana uwezo wa juu sana hivyo ni upekee wako katika kuwashawishi majaji ndio ulikuwa unakupa nafasi ya kuendelea.

 

ELIKANA YASSIN LIHUWI (28)

Ni mjasiriamali na mkazi wa Dar es Salaam. Nilipata taarifa ya Shindano hili kupitia ukurasa wa Instagram wa @ ericshigongo na @tonyinspirational.

Changamoto kubwa niliyoipata toka siku ya kwanza ni kulazimika kufunga ofisi ninayoitegemea kuendesha maisha yangu na ya wale walio tegemezi kwangu ili niweze kuhudhuria usahili katika hatua mbalimbali.

 

NPSC imenipa fursa ya kufahamiana na vijana wenzangu wengi wenye weledi katika nyanja mbalimabali, na pia imenipa uzoefu zaidi wa kuzungumza, nimejifunza vingi kupitia maoni chanya na hasi ya majaji wetu ambayo yamenijenga sana.

 

RADHIA OMARY JAMBI (24)

Ni mjasiriamali. Nilipata taarifa za shindano hili kupitia WhatsApp status ya rafiki yangu.

Safari ilikuwa njema japo katika kila jema changamoto haziepukiki, hivyo kulikuwepo na changamoto kama vile uoga.

Nimefanikiwa kupata marafiki wapya na kuongeza uelewa wangu kuhusu sanaa ya uzungumzaji mbele ya hadhara.

 

MASTIDIA DIONIS GAPI (28)

Taarifa za shindano nilizipata katika group la WhatsApp. Mchakato mzima wa shindano ulikuwa mzuri ila wenye ushindani mkubwa kwa sababu ya uwepo wa vijana wengi wenye uwezo mzuri japo hilo halikuniogopesha.

 

LILIAN PROCHES MALAMSHA (22)

Mara ya kwanza nilipata taarifa kuhusu shindano hilo kupitia kwa rafiki yangu. Katika shindano hili nimejifunza mambo mengi ambayo yamenijenga.

 

Sikutegemea kufika 30 bora, namshukuru Mungu sana kwa yote aliyonipitisha kwa kuwa kila mshiriki alikuwa na kitu cha ziada ambacho kilimpa uwezo wa kushinda. Shindano linafurahisha na kuchangamsha akili kwa ujumla.

Leave A Reply