The House of Favourite Newspapers

Watangazaji wa Kike… Wakali wa Taarifa ya Habari TV / Redioni

0
FARHIA MIDDLE- ITV.

UKITAMBUA na kuona ubora wa kazi anayoifanya mwenzako kisha kumwambia, basi atafanya zaidi ya ilivyotarajiwa. Tujifunze kukubali na kupongeza juhudi za wenzetu.

Binafsi ni mwanahabari kikazi, kitaaluma na maisha. Lakini huwa sisahau kupongeza kazi za waandishi wenzangu, hususan kwenye kipengele cha taarifa ya habari.

Kama ilivyo kwa tasnia nyingine, taarifa ya habari inao mkusanyiko wa watu lukuki wenye weledi katika kuhabarisha umma.

Wapo wanawake wengi ambao ni wasomaji wa taarifa ya habari na kutangaza vipindi mbalimbali runingani na redioni. Hapa nakuletea orodha ya watangazaji wa kike Bongo, ambao ni mahiri kwa kizazi hiki kwenye usomaji wa taarifa ya habari runingani na redioni.

FARHIA MIDDLE- ITV/ RADIO ONE

Alianza kujulikana zaidi baada ya kuanza kusoma taarifa ya habari Redio One na baadaye ITV, licha ya kuanzia kwenye vituo vingine mikoani ikiwemo Arusha na Manyara.

Farhia ni miongoni mwa watangazaji wa kike hapa Bongo kwa kizazi kipya, wajuzi na mahiri wa kusoma taarifa ya habari.

Muonekano wake ni wa kuvutia, lakini kikubwa ni namna matamshi yake yalivyo bora na kujiamini hususan kwa upande wa TV ambapo huonekana akiitawala studio.

Kingine kinachompa alama nyingi Farhia ni ule ubunifu na utundu wake wa kucheza na maneno ya Kiswahili kwani ndiye muasisi wa neno mubashara ambalo kwa siku za hivi karibuni limekuwa likitumika sana ndani na nje ya vyombo vya habari, likiwa na maana ya ana kwa ana (live).

Pia ni mtangazaji wa kwanza kulikuza neno arafa badala ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), hivyo anaibuka kuwa kinara katika orodha yangu.

FATMA ALMASI NYANGASA.

FATMA ALMASI NYANGASA – AZAM

Huyu naye ni mjuvi. Anajua na anaweza sana kusoma taarifa ya habari. Anabebwa na uzoefu, kwani ni miongoni mwa watangazaji wa kike waliokaa muda mrefu kwenye tasnia ya habari akianzia kung’ara akiwa ITV/ Radio One kabla ya kutimkia Azam miaka miwili iliyopita.

Fatma ana mvuto wa kipekee kwani tabasamu na uchangamfu wake pindi asomapo taarifa ya habari runingani hugeuka kivutio kikubwa kwa watazamaji hivyo kujiongezea umaarufu na hivyo ameweza kuingia kwenye orodha hii ya vinara.

GRACE KINGARAME (katikati).

GRACE KINGARAME – TBC1

Hababaiki na wala hapepesi macho. Yuko makini kuhakikisha kila herufi inatamkwa vyema mdomoni mwake na kuwafikia kwa usahihi watazamaji.

Upekee wa dada huyu ni usahihi wa matamshi yake, yaani panapostahili kuwekwa ‘L’ hukaa herufi hiyo na huitamka kwa ufundi unaovutia kwa namna ambayo sioni lugha nzuri ya kueleza.

Vivyohivyo na kwenye herufi ‘R’ kitu ambacho huwashinda watangazaji wengi hususan kwa kipindi hiki.

Grace amedumu muda mrefu TBC1, huu ni uthibitisho tosha kwamba anajua na kazi anaiweza.

ESTER AMANDUS ZELAMULA – CHANNEL TEN

Rangi na muonekano wake vinambeba. Lakini kikubwa zaidi ni namna ambavyo husoma kwa hatua na mapozi yenye kuvutia.

Hana haraka sana lakini ni mzingatiaji mzuri wa muda. Harudii maneno na kuchanganya sentensi kama ambavyo wengi wamekuwa wakifanya. Ester anajiamini sana.

Lakini kingine ni unadhifu wa mavazi yake. Anajipenda na anajua kupangilia mavazi kwa kuzingatia rangi, hivyo zinatosha kabisa kumuingiza kwenye orodha yangu.

MAHIJA ZAYUMBA –  CLOUDS TV

Uchangamfu na wepesi wake katika kupangilia habari unampa umaarufu. Anasoma harakaharaka lakini kwa umakini na kwa kusikika kwa watazamaji.

Mahija hana uzoefu mkubwa sana kwenye tasnia lakini ni moto wa kuotea mbali kwenye usomaji wa taarifa ya habari.

Naye anajiamini na pia ni nadhifu. Anatosha kujumuishwa kwenye kundi hili la dhahabu.

HAWA NAKUPA WA ZIADA

Hao niliokupa hapo juu ni kutokana na maoni ya Showbiz Extra, wapo pia wengine kama Ivona Kamuntu (Azam), Marry Edward (Channel Ten/ Magic FM), Jacqueline Silemu (ITV/ Radio One), Elizabeth Mramba (TBC1), Upendo Msuya (Channel Ten), Neema Kindole (ITV/ Radio One), Bahati Alex (ITV/ Radio One), Kisa Mwaipyana (Channel Ten), Nyamiti Kayora (Star TV/ RFA) na wengineo wengi ambao kwa kweli wanajua na kuipenda kazi yao.

BRIGHTON MASALU

Jaji Mkuu Afungukia Sakata la Tundu Lissu, Akataa Kujifananisha na Majaji wa Kenya

Leave A Reply