The House of Favourite Newspapers

Watanzania Waishio Nje Wachangia Mil. 22.3 Matibabu ya Lissu

0
Tundu Lissu.

Dar es Salaam — JUMLA ya Dola za Marekani 9,968 ambazo ni sawa na Sh. Millioni 22.3 za Tanzania, zimechangwa katika muda wa siku nne na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaoishi nje ya Tanzania ili kumpatia matibabu zaidi nchini Marekani, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye hivi sasa anatibiwa Nairobi, Kenya, baada ya kushambuliwa zaidi ya wiki moja iliyopita mjini Dodoma na watu wasiojulikana hadi leo.

Wafuasi hao wa Chadema walianzisha kampeni kwenye mtandao ambapo walitegemea kupata Dola 50,000 (Sh. 112m) ambazo zingewezesha kumsafirisha Lissu kwa ndege ili akatibiwe Marekani. Kutokana na mchango huo, chama hicho kinahitaji kupata Dola 40,032 (Sh. 89.6m) ili kufanikisha lengo hilo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji ndiye msimamizi wa michango hiyo. Lissu alisafirishwa kwenda Kenya kupata matibabu zaidi baada ya kujeruhiwa na risasi tano miongoni mwa risasi zaidi ya 32 zilizopigwa na washambulizi wake. Kwa mujibu wa viongozi wa chama chake waliomtembelea, hali ya Lissu inaendelea vyema.

Baada ya kushambuliwa akiwa anarejea nyumbani kwake eneo la Area D Dodoma, Lissu alikimbizwa Hospitali ya Dodoma alikopatiwa matibabu ya muda kabla ya kusafirishwa kwenda Nairobi kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha ya risasi yaliyompata kwenye miguu, tumboni na mkononi.

Leave A Reply