The House of Favourite Newspapers

WATATU WAUAWA MIKONONI MWA POLISI

UTATA mkubwa umeibuka kufuatia vifo vya vijana watatu waliotajwa kwa majina ya Ismail Linyembe, Twahir Said ‘Gama’ na Iddi Said wakazi wa Mbagala Kilungule jijini Dar ambao inadaiwa mauti yamewafika wakiwa kwenye mikono ya polisi, Ijumaa Wikienda lina habari hii ya kushtua.

Wakizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, baadhi ya watu wa karibu wa marehemu hao wamesimulia jinsi ndugu zao hao waliowaita ‘raia wema’ walivyotoweka katika mazingira ya kutatanisha kisha baadaye taarifa kutolewa kuwa, wameuawa na maiti zao ziko mochwari katika Hospitali ya Temeke jijini Dar.

Tumsikie kaka wa marehemu

Kaka wa marehemu Twahir aliyejitambulisha kwa jina la Khalid Chande akizungumza na Ijumaa Wikienda kwa uchungu alidai kuwa, Julai 8 mwaka huu, Iddi ambaye ni mpwa wake aligombana na mwenzake aitwaye Kashi, chanzo kikidaiwa ni simu na kumfanya Kashi kumjeruhi kwa panga la kichwani.

“Baada ya kujeruhiwa, damu nyingi zilianza kumtoka Idd, Kashi akatimka zake ndipo alipotokea Ismail Linyembe (marehemu) ambaye alikodi bodaboda na kumkimbiza kituo cha afya pale Mbagala Zakhiem,” alidai Khalid. Kaka huyo alizidi kudai kuwa, walipofika kwenye kituo hicho daktari waliyemkuta aliwaambia waende polisi wakachukue PF3 ndipo aweze kumtibu mgonjwa, vinginevyo asingeweza kumpa huduma.

“Baada ya kuambiwa hivyo, Ismail na Idd walielekea kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Charambe ambapo walipatiwa PF3 lakini waliporudi pale Zahanati walikuta askari wakiwasubiri ambapo baada ya kuwaona waliwakamata na kuwaingiza kwenye gari lao, madai ambayo polisi hawajakiri kuwachukua watu hao.

“Wakiwa eneo hilo, Twahir (ndugu wa marehemu Idd) alifika pale kwenye kituo hicho cha afya kwa ajili ya kupeleka pesa ya kusaidia matibabu lakini naye alikamatwa na kuunganishwa na wenzake, sababu za kukamatwa kwao hatujui,” alidai kaka huyo.

Ikadaiwa kuwa, wakati hayo yakifanyika dereva wa bodaboda aliyekuwa akiwazungusha Ismail na majeruhi huyo (Idd) alipoona wenzake wanakamatwa aliamua kuwasha bodaboda yake na kuondoka eneo hilo kisha kwenda nyumbani kwa waliokamatwa kutoa taarifa.

Ndugu huyo aliendelea kudai kuwa, tangu vijana hao wakamatwe Julai 8, mwaka huu, walianza kuwasaka maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye vituo vya polisi Nzasa, Charambe, Zakhem, Chang’ombe, Stakishari, Kituo Kikuu cha Kati (Sentro) pamoja na hospitali bila kuwaona wala kupata taarifa za kueleweka.

“Ukweli hali hiyo ilituchanganya sana lakini Alhamisi iliyopita tukiwa katika harakati za kuwasaka ndugu zetu kwenye Kituo cha Polisi cha Kizuiani ‘Maturubai’ alitokea afisa mmoja wa polisi, aliyeonekana ana cheo kwenye Mkoa wa Kipolisi wa Temeke na kutuambia ndugu zetu waliuawa na wananchi wenye hasira wakati wakitaka kuwatoroka polisi eneo la Beas na maiti zao ziko Hospitali ya Temeke.  “Taarifa hizo zilituchanganya sana. Hata hivyo tulimuomba afisa huyo akatuoneshe hilo eneo walipopigiwa ndugu zetu na hao wananchi wenye hasira ili nasi tukajiridhishe kwa maana alipopigiwa mtu hata kama ni jambazi hapana siri.

“Kwa kifupi hatukupa ushirikiano, tumebaki njia panda, hatujui ndugu zetu wamekufakufaje. “Tulichoamua sisi ni kwamba hatutakwenda kuchukua miili mpaka tujue kilicho nyuma ya vifo vyao, ikibidi tutakwenda Ikulu kumuona Rais Magufuli (John),” alisema Khalid.

MAMA WA ISMAIL AONGEA KWA UCHUNGU

Akizungumza na Wikienda, mama mzazi wa marehemu Ismail aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma Chinguile alisema amepokea taarifa za kifo cha mwanaye kwa mshtuko mkubwa na hajui nini kimesababisha uhai wake ukatizwe mapema wakati bado anamhitaji.

“Huyu ndiye mwanangu mkubwa niliyekuwa nikimtegemea katika maisha yangu lakini leo naletewa taarifa za kifo chake tena kimesababishwa na yeye kumsaidia mtu aliyepatwa na tatizo kumpeleka hospitali. “Maumivu niliyonayo hayaelezeki. Mimi naviomba tu vyombo vya sheria vifuatilie kujua nini kipo nyuma ya vifo vya watoto wetu hawa,” alisema mama huyo huku akitokwa na machozi.

MAMA TWAHIR ASHINDWA KUZUNGUMZA

Mwandishi wetu alijaribu kuzungumza na mama mzazi wa Twahir ambaye pia ni bibi wa Iddi lakini alishindwa kuzungumza na kubaki akilia muda wote huku akitaja jina la Rais Magufuli na kuomba awasaidie.

NDUGU WAGOMA KUZIKA MIILI

Baba mdogo wa marehemu Ismail aliyejitambulisha kwa jina la Shafii Linyembe alisema kuwa, hawatazika mwili wa marehemu huyo mpaka watakapopata maelezo ya kuridhisha na kujua hatua zitakazochukuliwa kuhusiana na tukio hilo.

“Mwili wa ndugu yetu hatuendi kuuzika mpaka tusikie kauli za viongozi watueleze ukweli wa nini kilitokea na ndugu yetu alikufa vipi ndipo tuweze kumzika,” alisema.

RPC AZUNGUMZA NA WIKIENDA

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Msaidizi, Emmanuel Lukula alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema bado hajafikishiwa mezani kwake na kuahidi kuzifuatilia.

“Hizo taarifa bado hazijanifikia mezani kwangu ndiyo kwanza nazisikia kwako, yaani tukio kubwa kama hilo linatokea halafu mimi sina taarifa, sijui ni kwa nini lakini nakuahidi nitalifuatilia muda si mrefu ila kwa sasa niko msibani na hivi tunavyoongea ndiyo tunataka kuelekea makaburini, asante sana kwa taarifa,” alisema kamanda huyo. Gazeti hili linafuatilia kwa karibu sakata hili kujua nini hasa kilitokea na kusababisha vifo vya vijana hao na tunaahidi kuwaletea kitakachojiri kupitia magazeti mengine ya Global Publishers.

Comments are closed.