The House of Favourite Newspapers

Waturuki Watua Kuijenga Upya Yanga

0

TAARIFA ilizozipata Spoti Xtra kutoka ndani ya Klabu ya Yanga zinasema kwamba, kampuni moja kutoka nchini Uturuki, hivi karibuni ilifika klabuni hapo kwa ajili ya kufanya vipimo vya Uwanja wa Kaunda ili kuufanyia makadirio kabla ya kuanza ujenzi.

 

Kwa muda mrefu, Yanga imekuwa katika mikakati ya kuukarabati uwanja huo ili uweze kutumika kwa mazoezi ya timu zao za vijana, wanawake na wakati mwingine ya wakubwa.

 

Mtoa taarifa huyo alilidokeza Spoti Xtra kwamba: “Ni hivi karibuni tu, Waturuki walikuja kuangalia namna gani wanaweza kuukarabati Uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika kama zamani.

“Yanga inataka kuukarabati uwanja huu utumike kwa mazoezi na baadhi ya mechi za vijana na timu yetu ya wanawake, Yanga Princess ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.”

 

Wakati Waturuki hao wakilenga zaidi kwenye uwanja, jumla ya shilingi milioni 180 zimetengwa kwa ajili ya kukarabati vyumba vya kulala kwenye Makao Makuu ya Klabu ya Yanga yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla, alisema jengo hilo lina jumla ya vyumba 30 na kila kimoja kukikarabati gharama yake ni shilingi milioni 6, kwa idadi ya vyumba, gharama kwa jumla ni shilingi milioni 180.

 

Msolla alisema kuwa ukarabati wa vyumba hivyo utafanywa na mashabiki na wanachama wapenda maendeleo watakaokuwa tayari kugharamia kila chumba huku wakiweka utaratibu wa kukipa jina chumba kwa yule atakayekarabati.

 

Alisema kuwa, Kamati ya Miundombinu iliyo chini ya mwenyekiti wake, Bahati Maseba, ndiyo iliyochukua jukumu hilo la ukarabati wa vyumba ambayo tayari imekarabati chumba kimoja cha mfano chenye hadhi na ubora kwa lengo la kupata makadirio ya fedha.

 

“Yanga tuna timu nne, gharama za kuziweka kambini kwa maana ya kulipia hoteli ni kubwa sana. Hivyo katika kupunguza gharama hizo tumeona ni vema tukakarabati jengo letu hili lililopo hapa klabuni.“

 

Tukishakarabati jengo letu timu zetu za U17, U20 na Yanga Princess zitakuwa zinakaa kwenye jengo letu zinapokuwa na mashindano kama ilivyokuwa kwa Yanga Princess ambayo hivi sasa ipo katika mashindano.

 

“Hadi kufikia muda huu baadhi ya viongozi kama Injinia Hersi Said, Lingalangala (Thobias) Arafat (Haji) kutoka Kamati ya Utendaji wenyewe kila mmoja amechukua chumba kwa ajili ya ukarabati.

 

“Pia wapo wengine kama Umoja wa Makundi ya WhastApp Kitaifa, wenyewe wamechukua vitano, Kamati ya Utendaji na Sekretarieti za timu zimechukua chumba kimoja kila moja, hivyo tunawaomba wanachama, mashabiki, makampuni na wadau wa soka kujitokeza katika ukarabati wa jengo hili,” alisema Msolla.

 

Kwa upande wa Masaba, alisema: “Tofauti na ukarabati wa vyumba, pia watakarabati bwawa la kuogelea na gym.“Baada ya kukamilisha ukarabati wa Jangwani, haraka projekti ya Kigamboni itaanza ya ujenzi wa uwanja, hosteli, mabwawa ya kuogelea, gym na ofisi, hivi sasa tupo katika hatua za mwishoni na hivi karibuni tutamtambulisha mkandarasi wa ujenzi huo.”

Stori: Wilbert Molandi, Dar

Leave A Reply