The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-28

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Sasa nenda na huyo askari, atakwenda kuandikisha maelezo yako halafu nitakuja kukukabidhi gari lako.”

Nikatoka na yule polisi. Tulikwenda kaunta ambako alitoa faili akaanza kuandikisha uongo wangu.

Baada ya kuandika jina langu, umri wangu na wadhifa wangu wa uwaziri, alitaka nimueleze jinsi gari hilo lilivyoibiwa.
Nilibuni tu jina la hoteli halafu nikamwambia.
SASA ENDELEA

“Nina kawaida ya kufika katika hoteli hiyo mara kwa mara pamoja na mke wangu.”
Nilisisitiza kumtaja mke wangu kwa sababu sikutaka nionekane nina tabia za kihuni. Waziri mzima kama mimi kwenda katika majumba ya starehe wakati wa usiku nikiwa peke yangu isingeleta picha nzuri.

“Mlifika saa ngapi?” Polisi huyo akaniuliza.
“Tulifika kama saa nne usiku!”
“Gari mliliacha wapi?”

“Katika eneo la kuegesha magari liliopo mbele ya hoteli.”
“Baada ya kuliacha hilo gari mkaingia ndani?”
“Ndiyo, tuliingia ndani.”

“Mlitoka saa ngapi na kukuta hilo gari limeibiwa?”
Nilijifanya kama ninayefikiri kisha nikajibu.
“Ilikuwa kama saa sita na nusu hivi.”

Nikakumbuka kuwa ofisini kwa mkuu wa kituo nilipoulizwa swali hilo nilisema nilifika hotelini hapo saa nne usiku.
“Kwa hiyo mlipotoka mlikuta hilo gari halipo?” Polisi huyo aliendelea kuniuliza bila kujua nilichokuwa ninawaza.

“Ndiyo, tulikuta halipo.”
“Mlitoa taarifa kwenye uongozi wa hoteli kwamba mmeibiwa gari lenu?”
Hilo swali lilinikwamisha. Kama polisi huyo aliyekuwa akinihoji angekuwa makini angegundua kuwa nilikuwa nimegwaya.

Swali hilo lilinikwamisha kwa sababu hilo tukio la mimi na mke wangu kufika katika hoteli hiyo halikuwepo. Na lilikuwa jambo la kawaida kwa mteja anapoibiwa kitu sehemu kama hiyo kutoa taarifa kwa uongozi wa mahali hapo. Kama ningesema nilitoa taarifa hiyo, nilishuku huenda polisi hao wangekwenda hotelini hapo kuuliza maswali.

Niliendelea kujiambia, kama ningejibu kuwa sikutoa taarifa ya kuibiwa kwa gari langu kwa uongozi wa hoteli hiyo ningeonekana muongo.
Katika sekunde hizo chache za kuulizwa swali hilo nilikuwa nikiilazimisha akili yangu kutoa jibu la haraka na lililostahiki.

Mara moja niliona paji la uso wangu likitanda tembe za jasho.
“Nilitoa taarifa kwa uongozi wa hoteli,” Niliamua kujibu hivyo ili nionekane mkweli.
“Uongozi wa hoteli ulikwambia nini?”

“Uongozi ulisikitika na nilitakiwa nitoe taarifa polisi…”
Nilipotaja neno polisi nilikumbuka kuwa sikuwa nimetoa taarifa katika kituo chochote cha polisi kwa vile tukio lenyewe halikuwepo.

“Lakini pia sikuwahi kwenda kupiga ripoti usiku ule…” nikajihami haraka.
“Hukwenda kupiga ripoti kituo chochote cha polisi?”
“Ilikuwa usiku mwingi, niliona nirudi nyumbani nije asubuhi.”

Polisi huyo alimaliza kuandika maelezo yangu na mimi nikashukuru kwa kukamilika kwa zoezi hilo.“Hebu soma haya maelezo niliyoandika, ni sahihi?” Polisi huyo aliniambia huku akinigeuzia lile faili ili niweze kusoma.

Niliyasoma yale maelezo haraka haraka, nikakuta kipengele ambacho sikukitaka kiwemo.

“Hapa umeandika nini?” nikamuuliza yule polisi ambaye alisogeza uso wake na kukisoma kipengele hicho kwa sauti ya kusikika.

“….niliuarifu uongozi wa hoteli kwamba gari langu limeibiwa lakini uongozi huo haukuchukua hatua yoyote zaidi ya kunitaka nitoe taarifa kituo cha polisi…”
“Siyo hivyo. Hapa ni kama ninaulaumu uongozi wa hoteli. Kwa kweli sipendi kuwalaumu, walisikitishwa na lile tukio…” nikamwambia.
“Ulitaka niandikeje mheshimiwa?”

“Kwamba nilitoa taarifa katika uongozi wa hoteli…uongozi ulisikitishwa sana na wakanitaka nitoe taarifa polisi.”

“Sawa mheshimiwa. Ngoja nirekebishe kipengele hicho.”
Baada ya polisi huyo kufanya marekebisho, alikwenda kumfahamisha mkuu wa kituo ambaye alitoka ofisini kwake akiwa ameshika lile kadi la gari langu.
“Umekuja na funguo ya lile gari?” akaniuliza.
“Ndiyo ninayo. ”

“Twende nikakukabidhi.”
Mimi na mkuu huyo wa kituo tulitoka nje ya kituo hicho na kwenda lilipokuwa gari hilo.
Tulilikagua gari kwa pamoja kisha nikajaribu kuliwasha. Gari liliwaka bila tatizo.

“Sasa mheshimiwa kama umeshatoa maelezo yako unaweza kuchukua gari lako, tutakapokuhitaji tutakuita,” mkuu huyo wa kituo akaniambia.

“Sawa”

Nilimuita yule dereva wa gari hilo nikamwambia alipeleke gari hilo nyumbani kwangu.
“Tafadhali usimueleze kitu chochote mke wangu” nikamwambia.
Wakati namwambia hivyo, mke wangu akanipigia simu hapo hapo.
“Hello… mke wangu niaje?” nikamuuliza.

“Umeondoka na gari gani?”
“Nimeondoka na gari lako. Gari la ofisini limepelekwa gereji lakini tayari nimempa dereva akuletee” nikamdanganya.
“Huyo dereva mlikutana wapi?”
“Nilimpigia simu kumuita ofisini kwangu, atakuja nalo sasa hivi”

ITAENDELEA

Leave A Reply