The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-40

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
Mara ileile tukamuona mlinzi akimfungulia geti dereva huyo aliyewasili muda uleule.
Mke wangu alipomuona alishuka haraka kwenye baraza ya nyumba, akaelekea kwenye gari letu.
Dereva alikuja kunisalimia kisha akaenda kwenye banda la gari. Kwa vile ufunguo wa gari hilo tunauacha ndani ya gari, alifungua mlango akajipakia na mke wangu naye alifungua mlango wa nyuma akajipakia na mwanaye.SASA ENDELEA…

Mimi na msichana huyo tulikuwa tunakubaliana kwa mengi lakini kwa hili lililotokea tayari tulikuwa watu mbalimbali. Ilikuwa wazi kuwa si tu mke wangu alikuwa anataka kumsalimisha mtoto wetu dhidi ya wale wachawi lakini pia alikuwa ananiogopa! Alishaona kuwa sikuwa mwenzake. Niliamini kwamba ile ilikuwa safari ya moja kwa moja na asingerudi tena kwangu.

Mara gari likatiwa moto. Mlinzi alifungua geti, gari hilo likatoka.
Nililisindikiza kwa macho hadi gari hilo lilipotoweka kwenye macho yangu baada ya geti hilo kufungwa. Nikarudi ndani.

Niliingia chumbani nikaketi kwenye kitanda na kujiinamia. Tukio lile lilikuwa limenihuzunisha sana na pia nilijua kuwa lingeniletea fedheha kubwa.
Nilijiuliza kama mke wangu amemueleza mama yake kuwa mimi ni mchawi na kwamba nilikuwa nataka kumtoa kafara mtoto wetu, yule mama atanielewaje? Au nitakuwa na uso gani wa kutazamana naye nitakapokwenda kwake?

Hata kama mamamkwe wangu hataamini kuwa mimi ni mchawi lakini mwanaye atakapomueleza kuwa aliufuma mkoba wangu wa uchawi uvunguni mwa kitanda ukiwa na mkono wa mtoto mchanga uliokaushwa, yule mama lazima ataamini.

Atakapoamini kuwa mimi ni mchawi tayari heshima yangu kwake itakuwa imeporomoka.
Ili kujiepusha na aibu, nilifikiria kuwa nisiende tena nyumbani kwa mamamkwe kwani sikuwa na uso wa kutazamana na mama huyo niliyekuwa nikimheshimu sana.

Ukweli ni kwamba siku ile sikwenda kwa mamamkwe kujitetea wala kujieleza vinginevyo. Nilijua pia kutokwenda kwangu kungewapa uthibitisho zaidi kuwa mimi ni mchawi.
Nilishindwa kwenda angalau kumtembelea mwanangu kwa sababu ya aibu. Ajabu ni kuwa usiku wa siku ile wale wachawi hawakufika nyumbani. Sikujua kama walishajua kuwa mtoto wangu hakuwepo na pia sikuweza kujua kama walimfuata huko alikopelekwa na mama yake.

Asubuhi kulipokucha nikampigia simu mke wangu ili kama wachawi hao walifika usiku anieleze.
Mke wangu alipopokea simu, akaniuliza.
“Umeona uchungu sana tulivyoondoka hapo nyumbani?”
“Kwa nini unaniuliza hivyo?”

“Naona tangu tulipoondoka jana unatukumbuka leo?”
“Kwa hapo ninakiri kosa, naomba unisamehe…” nikamwambia.
“Sawa.”
“Mamamkwe hajambo?”
“Hajambo.”

“Na mtoto naye hajambo?”
“Mungu bado anamsaidia, ataishi huyu kwa uwezo wa Mungu.”
“Unaponiambia hivyo ninaona kama unanishutumu mke wangu. Jana nilikueleza kila kitu kuhusu mimi lakini inaonekana hutaki kuniamini.”

“Sawa,” akaniambia kiunyonge.
“Nitakupigia tena baadaye, hivi sasa najiandaa kwenda kazini.”
“Sawa,” mke wangu akaniitikia tena. Niliona kama alinifanya sina akili.
Nikakata simu.

Jioni niliporudi kutoka kazini nilimpigia simu tena. Tukazungumza kidogo. Niligundua kuwa mke wangu alikuwa bado haniamini.
Nilitoka usiku nikaende kula chakula kwenye hoteli moja, niliporudi, nikalala.
Nilikuja kuamshwa saa tisa usiku kwa mlio wa simu. Nilipopokea simu nilishtuka kusikia sauti ya mke wangu.

“Baba Mkanga mbona unanifanyia hivi?” mke wangu akaniuliza kwa sauti ya uchungu.
“Nakufanyia vipi?” nikamuuliza kwa wasiwasi.
“Watu wako si wamekuja hapa nyumbani, wameingia hadi ukumbini wanasema wanamtaka mtoto wao!”
Nilishtuka sana niliposikia maneno yale.

“Wameondoka au bado wapo?” nikamuuliza kwa haraka.
“Wameondoka lakini wamepiga kelele sana wakacheza ngoma zao hapo ukumbini.
Wamesema kesho wanakuja kumchukua mtoto wao. Mama yangu pia ameshangaa. Nilidhani nikiondoka huko yataisha, kumbe wamenifuata hadi huku! Sasa nitafanyaje jamani!”

“Lakini mimi sihusiki na watu hao. Wanajaribu kusema uongo ili kutuletea mtafaruku.”
“Mimi nazungumzia huyu mtoto, kwa nini wanataka wamchukue?” Hapo mke wangu aliniuliza kwa hasira.

Sikuwa na jibu la haraka, akaniambia.
“Sasa kesho uje hapa nyumbani, mama anakuita. Utakapokuja uje na ule mkoba wako.”Kabla sijajibu kitu mke wangu akakata simu.
Asubuhi yake ilikuwa ni Jumapili. Nikaona lile suala ni lazima nilipeleke kwa mchungaji, vinginevyo nitaumbuka.

Siku ile nilikwenda kwenye ibada ingawa siku nyingine nilikuwa sionekani. Baada ya ibada ya asubuhi nikamueleza mchungaji kuwa nilikuwa na mazungumzo naye lakini nilitaka mazungumzo hayo yafanyike nyumbani kwangu.

Je, nini kitaendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply