The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi

0

ILIPOISHIA IJUMAA:

“Alah! Wale watu wamepotelea wapi?” Dereva akaniuliza kwa mshangao wakati gari likiwa kwenye kasi.
“Si nilikwambia pale hapakuwa na watu, ni maroroso matupu.”
“Ni kweli ulivyosema, umejuaje?”
“Sote tumezaliwa humuhumu, tutakosaje kujua hulka zetu?”
SASA ENDELEA…

Kila mara dereva wangu alikuwa akitazama nyuma. Alionesha wazi kuwa alikuwa amepata uoga.

“Mpaka sasa sijaelewa. Kama wale walikuwa si watu, walikuwa akina nani?” akaniuliza.
“Ni uchawi?”
“Sasa kwa nini uchawi huo ututokee sisi?”
Nikaona maswali yatakuwa mengi, nikamjibu nilivyojisikia kumjibu.

“Wanatega tu uchawi wao ili kusumbua madereva wanaopita katika njia hii.”
“Hii ndiyo mara yangu ya kwanza kuona vitu kama hivi.”
Nikanyamaza kimya. Baada ya kimya kifupi, akaendelea kusema.
“Kama si wewe ningesubiri palepale hadi jua lingekuchwa.”
Nikazuga. “Watu wengine wanataka kusumbua watu tu.”
Baada ya hapo tukawa kimya.

Japokuwa dereva wangu alinyamaza, niliamini alikuwa akiendelea kulifikiria lile tukio.
Tuliendelea na safari hadi tukafika Dar.
Tulifika Dar usiku. Dereva alinipeleka nyumbani kwangu kisha akarudisha gari wizarani.
Nilishukuru kwamba tulifika salama Dar. Kina Bi Shali walikuwa wametupangia mkakati wa kutukwamisha njiani na pengine kutuua kabisa.

Kwa vile walikuwa na chuki na mimi baada ya kuwaagiza polisi wakawaweke ndani, waliona na wao wanikomeshe. Jambo moja tu walilisahau kuwa na mimi ni mwenzao, wasingeweza kunipata kirahisi.

Mkosi wao ulianza pale dereva wangu alipogonga mtu na kusababisha tupoteze muda mwingi tukiwa kituo cha polisi.
Kama haikutosha, walipasua tairi la gari langu ili kutupindua lakini hatukupinduka. Mwisho wao ulikuwa ni ule wa kutusimamisha barabarani tukidhani tunapisha watu wanaokwenda kuzika kumbe hakukuwa na kitu.
Kama nisingewashtukia mapema, sijui ingekuwaje!
Lakini niliona wazee hao walikuwa wanajidanganya wakidhani kuwa wangeweza kunikomoa wakati kule walikokuwa na mimi nilitokea hukohuko.

Baada ya siku ile, niliendelea kubaki Dar. Nilikuwa nikifanya ziara mbalimbali za kikazi mikoani ambapo niliwahi pia kufika Nzega lakini kule kijijini kwetu sikufika. Nilijua wale wazee wakiniona wangeniletea shida.
Siku moja wakati naamka asubuhi, mke wangu aliniambia kitu kilichonishtua kidogo.
Aliniambia kuwa alihisi alikuwa na ujauzito.

“Sikuona siku zangu mwezi uliopita na tayari naona nina kitu ndani ya tumbo langu,” akaniammbia.
“Mh! Hicho kitu unachokiona wewe ndiyo mimba?” nikamuuliza.
“Ndiyo, ni mimba. Hebu shika uone.”

Mke wangu aliushika mkono wangu akauminyisha chini ya tumbo lake na kuniambia.
“Unaona kitu kigumu hapa upande wa kulia?”
“Ndiyo, naona ni pagumu.”
“Ndiyo hapo.”

Hapohapo nikaikumbuka ile ahadi yangu na wale wachawi wa Nzega ambao nilikubaliana nao kuwa mtoto wangu wa kwanza niwape wao wamlee.
Nikajiambia kimoyomoyo.” Sitawapa mtoto yeyote.”
“Mbona umeduwaa?” mke wangu akaniuliza.
“Hapana. Nilikuwa nafikiria ujio wa mtoto wetu, sijui atakuwa mume au mke?” nikazuga ili mke wangu asijue nilikuwa nawaza nini.

“Wewe unataka mtoto gani?”
“Aanze mume?”
“Kumbe tuna mawazo tofauti!”
“Wewe unataka mwanamke?”

“Ndiyo, nataka nianze kuzaa mtoto wa kike halafu wafuatie wanaume.”
“Mimi nataka uanze kuzaa mwanaume.”
“Basi tumuachie Mungu atuamulie.”
“Ukizaa mwanaume hutafurahi?”
“Nitafurahi kama ndivyo Mungu alivyotaka.”
“Nakutania tu, mimi siangalii jinsia ya mtoto. Mtoto yeyote atakayezaliwa ni wangu tu.”
“Wewe tena…!”

Mke wangu akanicheka kwa kuona nilikuwa kigeugeu.
Sasa tukawa tunakuza mimba ya mtoto wetu. Kila nilipoliona tumbo la mke wangu likizidi kukua, nilikuwa nikifurahi.
Laiti ningejua matatizo ambayo yangekuja kunitokea baada ya mtoto huyo kuzaliwa, katu nisingefurahia mke wangu kupata ujauzito.

Leave A Reply