The House of Favourite Newspapers

Waziri Mbarawa Kutoa Ushahidi Mahakamani

0

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, anatarajia kutoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi inayomkabili mfanyabiashara Wilfred Massawe anayedaiwa kujipatia fedha kwa kutumia jina la waziri huyo.

 

Massawe anakabiliwa na mashitaka manne yakiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kujifanya yeye ni Profesa Mbarawa kipindi hicho akiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pia alijitambulisha kwa Waziri Kindamba ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuwa yeye ni Profesa Mbarawa.

 

Kesi hiyo ambayo ipo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ali, inaendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, na tayari mashahidi sita wameshatoa ushahidi wao.

Wakili Simon amedai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba wamebakiwa na shahidi mmoja ambaye ni Profesa Mbarawa.

 

Wakili Wankyo ameomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa ili shahidi huyo aweze kufika mahakamani. Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19, 2019 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

 

Katika kesi hiyo namba 3/2017 Massawe anadaiwa Novemba 25, 2016 akiwa maeneo ya Yombo-Buza Temeke jijini Dar es Salaam, alijitambulisha kwa Alfred Samson kwamba yeye ni Profesa Makame Mbarawa.

 

Katika mashitaka ya pili, inadaiwa Novemba 26, mwaka na mahali hapo, Massawe alijitambulisha kwa Izack Mwawima kuwa yeye ni Profesa Mbarawa. Inadaiwa mshitakiwa huyo pia alijitambulisha kwa Waziri Kindamba kuwa yeye ni Profesa Mbarawa.

 

Katika mashitaka ya nne, inadaiwa Novemba 25, 2016 maeneo ya Yombo-Buza Temeke, Massawe alijipatia Sh 700,000 kutoka kwa Samson baada ya alijitambulisha kuwa yeye ni Profesa Mbarawa wakati huo akiwa Wizara ya Ujenzi akiomba fedha hizo kwa ajili ya kusaidia mazishi,  udanganyifu alioufanya kwa njia ya mtandao.

Leave A Reply