The House of Favourite Newspapers

Hali ya Mbowe Bado ni Tete, Mahakama Yashindwa Kuendelea na Kesi

0

 

KESI ya uchochezi inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na mshtakiwa wa kwanza Freeman Mbowe kudaiwa bado afya yake si nzuri na anatakiwa kuonana na daktari.

 

Mbowe ambaye wiki iliyopita aliripotiwa kuugua na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jana alifika mahakamani hapo lakini kupitia wakili wake Peter Kibatala alieleza kuwa bado Mbowe hayupo vizuri kiafya na anahitaji kuonana na daktari kwa ajili ya uangalizi wa afya yake.

 

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa mashtaka nchini, Joseph Pande alidai kuwa Novemba 22 mwaka huu waliambiwa mshtakiwa Mbowe ametolewa hospitali na Novemba 26,2019 kesi ikaaharishwa kutokana na mshtakiwa huyo kutosijikia vizuri.

 

“Inashangaza leo (jana) mnakuja tena na hoja hiyo kwamba mshtakiwa anatakiwa kuonana na daktari, hayo yalitakiwa kusemwa tarehe tuliyokuwa tunaahirisha kesi,  hivyo hoja hiyo imepitwa na wakati kwani Novemba 27 mwaka huu nimemuona Mbowe akiendelea na kazi zake za chama kama kawaida,” alidai Panda.

 

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  alisema kuwa wanatakiwa kuwa makini na kesi hiyo kwani wasipofanya hivyo watajikuta wanaahirisha shauri hilo kila mara na haitaweza kumalizika.

 

“Nawaomba tuwe serious (makini) kwani kesi hii ipo hapa mahakamani muda mrefu inapaswa kuisha lakini washtakiwa wengine wanatoka maeneo mbalimbali ya hapa nchini,” alisema Hakimu Simba.

 

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo kwa siku ya jana na leo itaendelea kama kawaida ambapo itakuja kwa ajili ya kusikilizwa.

 

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

 

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.

Leave A Reply