The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Atoa Siku 3 Mafuta ya Kula Yapatikane – Video

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa kampuni za mafuta ya kula nchini kuingiza bidhaa hiyo sokoni na kuonya kuwa baada ya muda huo kupita, Serikali itapita viwandani na katika bohari za mafuta kufanya tathmini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo jioni Mei 9, 2018 bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye jana aliitaka Serikali kutoa majibu kuhusu madai ya kupanda kwa bei ya mafuta baada ya baadhi ya wabunge kuhoji jambo hilo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kutoa majibu ambayo hayakumridhisha.
“Serikali tunatoa siku tatu kuanzia kesho kwa mafuta yote yaliyoko katika bohari kuu ambayo tunajua yapo ili Watanzania wasihangaike kununua kwa bei ya juu, mafuta yaliyoko bandarini yanaendelea na taratibu zake,”amesema Majaliwa.
Amesema Serikali itaendelea kuzungumza na wafanyabiashara walio na mafuta bandarini kuondoa mafuta yao ili yaweze kusambaa sokoni ili watu wapate mafuta.
“Kuanzia Jumapili tutalazimika kuingia viwandani na kuhakiki kama mafuta yapo ama hayapo,”amesema.
Awali, Mwijage amesema mahitaji ya mafuta nchini ni kati ya tani 400,000 hadi 450,000 na kwamba vyanzo vya mafuta nchini vinatosheleza asilimia 30 ya mahitaji huku asilimia 70 ikiagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ni yaliyosafishwa na yale ambayo hayajasafishwa.
Amesema mwaka jana kampuni binafsi ambazo ndizo zinazoingiza mafuta kwa ajili ya kusafisha katika viwanda vilivyoko nchini, yaliingiza tani 344,369.5 ikiwa ni wastani wa tani 28,697 kwa mwezi.
Amesema Januari hadi Machi, 2018 kiasi kilichoagizwa cha mafuta kutoka nje ya nchi ni tani 30,210.71 na kwamba kwenye hifadhi kuna tani 68, 902 za mafuta.

VIDEO: MSIKIE MAJALIWA AKITOA AGIZO HILO

Comments are closed.