The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Awachimba Mkwara Mawaziri Kutoa Matamko Yasiyotekelezeka

0
Waziri Mkuu Majaliwa akiongea na Mawaziri wake.

Mawaziri na manaibu wao, wametakiwa kujiepusha na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko serikalini. Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana Jumanne, Novemba 7, 2017 alipofungua kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni vyema  viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara zao.

Pia, amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.

“Tunao wajibu wa kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais  Magufuli na wananchi wote kwa jumla,” amesema.

Waziri mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, utaratibu na kanuni.

Pia, amewataka wafanye ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya serikali.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mawaziri na manaibu wao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Viongozi hao pia wametakiwa kusimamia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply