The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu mgeni rasmi Stars vs Uganda

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

 

KAMATI ya Saidia Stars Ishinde chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda, imemwalika Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Uganda utakaocheza keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Mchezo huo ni wa kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) zinazotarajiwa kufanyika nchini Misri, mwaka huu.

 

Kamati hiyo ya uhamasishaji chini ya Makonda, imewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia Stars kuhakikisha inafanikiwa kufuzu nafasi hiyo ili kuweka rekodi ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda.

Mbali ya wanakamati kuzungumza na kutoa hamasa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Jengo la Mwalimu Nyerere, Posta jijini Dar es Salaam, jana, pia kuna watu wengine maarufu na wadau mbalimbali walipata nafasi ya kutoa maoni yao na kutoa hamasa kwa mashabiki.

 

“Mgeni rasmi katika mchezo huu atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nimeshazungumza naye na tayari amekubali ombi hilo, tunaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi uwanjani kuweza kuisapoti timu yetu.

 

“Nimeamua kununua tiketi 100 kwa ajili ya kuzipeleka kwenye vituo vya watoto yatima ili wapate nafasi ya kuja kushuhudia mchezo huo, mpira ni pesa tumeweza kumuona Samatta anaiingizia kipato familia yake pia watu wake wa karibu, hivyo tukiingia Afcon itaipeleka Tanzania katika ramani ya mpira,” alisema Makonda.

 

Baadhi ya waliotoa maoni ni Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Salehe Ally, wasanii wa filamu Jacob Steven ‘JB’ Jaqueline Wolper, Wema Sepetu, Steve Nyerere na watangazaji Shafii Dauda na Salama Jabir.

 

Wadau wengine ni Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’, Haji Manara, Edo Kumwembe na Said Tully.

Aidha, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema: “Kiingilio cha mchezo huo kitakuwa shilingi 2,000 kwa mzunguko, Sh 10,000 VIP B, Sh 20,000 kwa VIP A na Platinum ambayo ipo mara mbili ya Sh 100,000 na Sh 70,000.”

Comments are closed.