The House of Favourite Newspapers

Waziri Mpango Awasilisha Mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti

0

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.

 

 

“Pamoja na changamoto mbalimbali zilizoikumba Dunia ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara, kuendelea kukua kwa uchumi kumetokana na utekelezaji wa sera za bajeti na fedha chini ya uongozi thabiti wa Jemedari wetu JPM.

 

 

“Katika kipindi cha January hadi September, 2020, Pato la Taifa lilikua kwa 4.7%, aidha mfumuko wa bei ulifikia wastani wa 3.5% January 2021 ikilinganishwa na 3.7% January 2020.

 

 

“Riba za amana kwa kipindi cha mwaka mmoja zilipungua kufikia 8.41% December 2020 kutoka 8.90% December 2019 na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja imepungua na kufikia wastani wa 15.72% December 2020 kutoka 16.28% December 2019.

 

 

“Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine Duniani imeendelea kuwa tulivu kutokana na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti pamoja na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya Nchi.

 

 

“Hadi December 2020, deni la Serikali lilikuwa Tsh.Trilioni 59.0, sawa na ongezeko la 7.6% ikilinganishwa na Tsh.Trilioni 54.8 kipindi kama hicho mwaka 2019, kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Tsh. Trilioni 42.8 na deni la ndani ni Tsh. Trilioni 16.2.

 

 

“Ongezeko la deni la Serikali limetokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji; na malimbikizo ya riba ya deni la nje.

 

 

“Matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa iliyofanyika Desemba 2020 yanaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu,” Waziri Dkt. Mpango.

Leave A Reply