The House of Favourite Newspapers

Waziri Mpango Mgeni Rasmi Siku ya Takwimu Afrika Kesho

mpango-1
Meneja Takwimu za Pato la Taifa (NBS), Daniel Masolwa, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).

mpango-2
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

WAZIRI wa Fedha Dk. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika kesho ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yataanza saa tatu asubuhi ambapo wadau mbalimbali wa masuala ya takwimu na wananchi wanakaribishwa kuhudhuria.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Meneja Takwimu za Pato la Taifa (NBS), Daniel Masolwa, alisema maadhimisho hayo ni muhimu katika kupanga maendeleo na kutunga sera katika bara la Afrika.

Kauli-mbiu yake mwaka huu ni “Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu”.

Masolwa alisema lengo kuu la kuadhimisha siku hiyo ni kuongeza uelewa mpana kwa watumiaji wote wa takwimu Afrika kuhusu umuhimu wake katika kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote za kijamii na kiuchumi katika Bara la Afrika.

Alifafanua kwamba siku hiyo hutoa fursa kwa nchi kutathmini na kufuatilia malengo yaliyofikiwa katika mipango ya maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

Masolwa aliongeza kuwa umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za kiuchumi na zenye ubora kwa utangamano wa kikanda barani Afrika utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kufanikisha malengo endelevu, Agenda 2063 ya Afrika na mipango ya kitaifa ya kukuza uchumi.

Na Denis Mtima/Gpl

halotel-strip-2

Comments are closed.