The House of Favourite Newspapers

We baba fanueliii!!!-17

0

ILIPOISHIA

“Hapa safi, kama kazi imefanyika, hukuniangusha mzee mwenzangu,” alisema baba Fanueli.

“Usijali! Kwa hiyo inakuwaje?”

“Ndiyo nafikiria nini cha kufanya, kwanza ngoja, nitamfuata mimi mwenyewe kuzungumza naye, nikimwambia kuhusu hizi picha, atakoma na roho yake,” alisema mzee Paulo, akarushiwa zile picha kwa ‘bluetooth’ kisha kuondoka huku akiwa na hamu ya kuonana na mama Zubeda ili akinukishe.

TAMBAA NAYO

Hicho ndicho alichokitaka, kupata picha za mwanamke yule kwa kuamini kwamba naye angelipiza kisasi kutokana na kuharibiwa kwa mkewe mpaka kusababisha ugomvi mkubwa.

“Alijua?” aliuliza baba Fanueli.

“Angejuaje sasa? Hizi picha zimepigwa kimafia sana…” alijibu mzee Paulo huku akitoa kicheko cha chini, miongoni mwa watu waliojiona mashujaa, yeye alikuwa mmojawapo.

“Nashukuru sana, sasa hapa kazi kwangu,” alisema baba Fanueli, hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, huyoo akaondoka zake.

Njia nzima aliwaza kuhusu mama Zubeda, alimchukia kutoka moyoni mwake, alimchukulia kama adui namba moja katika maisha yake, kitendo cha kupata zile picha kikampa nguvu ya kumteketeza adui yake.

“Mbona upo hivyo?” aliuliza mkewe.

“Nipo vipi?”
“Unaonekana una furaha sana, kulikoni?”

“Hakuna kitu. Ngoja kwanza nipumzike,” alisema baba Fanueli.

Hakutaka kutoka, kitu alichokifikiria zaidi ni namna ya kukamilisha mpango ule aliokuwa nao, kummaliza mama Zubeda na kufanya yake.

Usiku alilala huku moyo wake ukiwa na amani mno, hata haki kwa mkewe aliitoa kama jinsi ilivyotakiwa kuwa, yaani ilikuwa ni kama siku za uchumba wao.

“Leo una nini mume wangu?” aliuliza mama Fanueli.

“Mbona kawaida tu, hakuna kitu.”

“Hapana! Unanificha!”

“Nikufiche ili iweje? Kama nikikuficha wewe! Sasa nani nitamwambia ukweli?”

“Mmmh! Sawa.”
Hakutaka kuweka wazi juu ya furaha yake, alichokitaka ni kufanya mambo yake kimyakimya.

Siku iliyofuata, asubuhi na mapema akajiandaa, safari aliyotaka kuifanya ni kwenda kwa mama Zubeda kwa lengo la kumtambia, alijua fika kwamba mwanamke huyo asingeweza kukurupuka kabisa.

Alipofika, akamkuta mwanamke huyo akiwa nje anafua huku pembeni kukiwa na wanawake wengine wakipiga stori.

“Habari yako!” alimsalimia.

Mama Zubeda hakuitikia, akamwangalia mzee huyo kuanzia chini mpaka juu, kisha akamrudisha, hakuridhika, akamnyali.

“Jamani si ninakusalimia!”

“Salama!”

“Sawa! Naweza kuongea nawe?”

“Uongee nami? Kuna nini?”

“Mazungumzo ya kawaida tu.”

“Na mimi unitongoze kama wengine?”

“Jamani! Mbona unakuwa hivyo? Kuna tatizo kuongea nawe?”

“Naomba uniache, hivi unafikiri nilijisikia vizuri uliponifukuza nyumbani kwako?”

“Kumbe tatizo ndo’ hilo?’

“Unaona zuri?”

“Tunaweza kuzungumzia kiutu uzima, tukamaliza kiutuuzima pia, naomba tukakae kwenye kivuli,” alisema baba Fanueli, muda wote uso wake ulionesha tabasamu pana.

Japokuwa mama Zubeda alikasirika ila hakuwa na jinsi, kwa sababu mzee huyo alifika kwake akiwa mnyenyekevu, akaamua kumkubalia na kwenda naye pembeni kwa ajili ya kuongea, ila pamoja na hayo yote, sura ya mwanamke huyo ilionesha ni jinsi gani hakuridhishwa na uwepo wa mwanaume huyo mbele yake.

“Naomba nikuulize kitu kimoja,” alisema baba Fanueli.

“Kuhusu nini?”

“Kwa nini ulikwenda kumwambia mke wangu umbeya mpaka ukasababisha akapigana na mwanamke mwenzake?” aliuliza baba Fanueli kwa sauti ya upole.

“Umbeya gani?”
“Kwamba natembea na kale kabinti.”

“Kwani uongo? Mbona kila mtu anajua hilo.”
“Sawa. Ila kibusara unatakiwa kuniomba msamaha!”

“Nikuombe msamaha wewe?”

“Ndiyo! Kwani kuna ubaya? Si wewe ndiye uliyenikosea kwa sababu haukuwa na ushahidi,” alisema baba Fanueli.

“Hahah! Haloo…eti sina ushahidi.”

“Unao?”

“Ili iweje.”
       “Sawa. Ila mbona wewe unatembea na wanaume wa watu na hatusemi kitu,” alisema baba Fanueli.

“Nitembee na wanaume wa watu! Mimi?”

“Ndiyo! Kwani naongea na nani hapa?”

“Una ushahidi?”

“Ninao, ila nitataka nimuoneshee mumeo na watu wengine wa mtaani,” alisema baba Fanueli.

“Heheh! Haloo…”

“Sawa! Subiri!”

Alichokifanya baba Fanueli ni kumsogelea kisha kutoa simu yake mfukoni, akaenda sehemu ya picha kisha kuzifungua zile picha alizotumiwa na mzee Paulo kisha kumuonesha, mama Zubeda akashtuka mno.

“Eeeh!” alijikuta akihamaki.

“Usihamaki! Kama ulivyokuja kuniharibia kwa mke wangu! Na mimi nakuharibia ili tuwe ngoma droo,” alisema baba Fanueli na kuanza kuondoka, mama Zubeda hakuweza kubaki, akaanza kumsogelea mzee huyo na kuanza kumuomba asifanye alichotaka kufanya, cha zaidi, akapiga magoti na kuanza kulia kama mtoto. Watu wote wakashangaa.

Leave A Reply