The House of Favourite Newspapers

Yanga Haina Pengo la Djuma Wala Aucho, Nendeni Uwanjani

0

YANGA inacheza mchezo muhimu sana keshokutwa wakati itakapokuwa ikivaana na Rivers ya nchini Nigeria.Huu ni mchezo muhimu kwa Yanga kuliko wenyewe wanavyofikiri kwa kuwa utakuwa na presha kubwa sana kwao.

 

Mchezo wa mwisho ambao mashabiki wa Yanga waliuona ni ule dhidi ya Zanaco wa siku ya Mwananchi ambao pia mashabiki wake hawakufurahishwa na matokeo yake.

 

Huu ni mchezo ambao mashabiki wanakwenda uwanjani wakibahatisha kama Yanga watafanya vizuri au watafanya vibaya, lakini ukweli ni kwamba utatumika kwa sehemu kubwa kupima ukubwa wa Yanga.

 

Yanga baada ya kurejea kwenye michuano ya kimataifa, kila shabiki alikuwa na hamu kubwa ya kuwaona wanafika mbali, shabiki alikuwa anataka kuwaona wanamfuta machozi ya misimu kadhaa nyuma kutokana na kuzomewa na mashabiki wa Simba kutokana na mafanikio ambayo timu yao imekuwa ikiyapata.

 

Nafikiri huu utakuwa mchezo muhimu zaidi kwao kuonyesha kuwa wanaweza kufanya vizuri na wanaweza kutikisa kwenye michuano ya kimataifa kwa sasa.

 

Lakini jambo moja ambalo naliona kwa Yanga, kwanza wenyewe hawajawa makini sana na mchezo huu, suala la kuja siku ya mwisho kuwaambia mashabiki kuwa watawakosa wachezaji wao watatu ni moja ya tatizo hilo.

Hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara kwa timu za Tanzania kwa wachezaji wao kukosa ITC na ukiwatazama wengi wanakuwa ni wale ambao hawakusajiliwa moja kwa moja, yaani usajili wao haukuhusu zaidi klabu zaidi ya mchezaji mwenyewe, au unaweza kusema wachezaji huru.

 

Hili limekuwa tatizo kubwa sana kwetu na kama hatutaliangalia vyema kuna siku timu itawakosa wachezaji hata kumi kwenye mchezo mmoja.

 

Kwa kiwango ambacho kilionyeshwa na Djuma Shaabani kwenye mchezo wa siku ya Mwananchi ni dhahiri kuwa mashabiki walikuwa wanatamani kumuona tena keshokutwa akiwa uwanjani.Ni dhahiri kuwa mashabiki walitaka kuona kama kweli anaweza kuonyesha ubora ule kwenye mchezo mkubwa dhidi ya Rivers.

Lakini kwangu naona ni nafasi ya pekee ya kumuona tena Kibwana Shomary akiwika, ni nafasi yake ya kuwaonyesha kuwa hakukuwa na ulazima wa kumsajili Djuma kwenye nafasi yake.

 

Kwangu naamini kuwa Kibwana hadi msimu uliomalizika unapita ndiye alikuwa mchezaji bora zaidi kwenye timu ya taifa, hii itakuwa nafasi yake ya kuwaonyesha kuwa anastahili kubaki kwenye nafasi yake pamoja na ubora wa Djuma.

 

Lakini pia sina shaka sana na nafasi ya Fiston Mayele kwa kuwa Makambo alishaonyesha kiwango chake, Makambo anatakiwa kudhihirisha kile ambacho alionyesha kwenye siku ya Mwanachi na shida kubwa kwake ni kwa kuwa mashabiki wanaamini kuwa yeye ndiye mchezaji wao bora.

 

Kwa upande wa Khalid Aucho, sina shaka napo hata kidogo, Mukoko Tonombe, Zawadi Mauya na hata ikishindikana Fei Toto mmoja wao anaweza kucheza kwenye nafasi hiyo.

 

Naamini kuwa kocha wa Yanga anaweza kumpa nafasi kubwa Mukoko, kwangu naamini anaweza kuwa nembo sahihi ya Yanga kwenye mchezo huu, nafikiri mashabiki wasiwe na shaka na timu yao.

STORI NA  PHILLIP NKINI – Ni Mtazamo Wangu

Leave A Reply