The House of Favourite Newspapers

Yanga hakuna kulala

0

IMG_1533YANGA ipo kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 19 katika mechi saba ilizocheza ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi kama hizo isipokuwa tofauti ipo kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.

Hadi inakaa kileleni Yanga imefunga mabao 18 na kufungwa matatu wakati Azam imefunga mabao 11 na kuruhusu matatu kama wapinzani wao.

Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm ameichungulia Azam na kusema ili wasiwafikie na kuwapita, amepanga mkakati wa kushinda kila mechi na kwa kuanzia mipango imebadilika katika maandalizi ya kila mechi.

3Pluijm raia wa Uholanzi aliliambia Championi Jumamosi, sasa hakuna haja ya kuzubaa hata kama wakipata ushindi leo kesho mazoezi ni kama kawaida ili wachezaji wake wawe fiti zaidi.

Kwa kawaida timu nyingi za ligi kuu hutoa muda wa mapumziko wa saa 24 kwa wachezaji wake kila wanapomaliza mechi kisha hukutana tena kwa maandalizi ya mchezo ujao.

Yanga ilipotoka kucheza na Toto Africans Jumatano iliyopita ambapo ilishinda mabao 4-1, kesho yake yaani juzi Alhamisi asubuhi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume kujiandaa na mechi dhidi ya Mwadui FC.

“Hatuna muda wa kusubiri, ligi ni ngumu sana, kila mechi kwetu ni kama fainali na kila timu inatubana inavyoweza hivyo hatupaswi kulala hata kidogo. Lazima tupambane, ndiyo maana hatukupumzika baada ya kucheza naToto.

Ili kuthibitisha kwamba hataki utani, Pluijm amepeleka kwa uongozi wazo la kutaka kesho Jumapili timu iondoke asubuhi kabla ya saa 4:00 kwenda Shinyanga kujiandaa na mechi dhidi ya Mwadui itakayochezwa Jumatano ya Oktoba 28, mwaka huu.

Kesho Jumapili ni siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na wachezaji wengi wa Yanga wana haki ya kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika kote nchini.

“Nataka timu iondoke Jumapili asubuhi, nimesikia kuna mambo ya uchaguzi, nimeomba wachezaji wapige kura mapema sana halafu tuondoke lakini kuwezekana kwa hili kunategemea na uongozi.

“Unajua wachezaji lazima watambue kuwa soka ndiyo ajira yao, pia wana haki ya kupiga kura hivyo wanatakiwa kuthamini vyote viwili kwa wakati, mechi inayokuja ni ngumu sana lazima tuwe makini,” alisema.

Hadi jana mchana, uongozi wa Yanga ulikuwa umebariki wachezaji kupiga kura kwanza ndipo waondoke kwenda Shinyanga kujiandaa na mechi dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage.

Tayari Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema anataka kutibua rekodi ya Yanga ya kutofungwa katika ligi kuu hadi sasa na kudai uwezo wa kufanya hivyo anao.

“Tunajiandaa kutibua rekodi ya Yanga ya kutofungwa japokuwa wana timu nzuri,” alisema Julio ambaye timu yake juzi Alhamisi iliifunga Majimaji mabao 3-0 huku mawili yakifungwa na Jerry Tegete aliyetoka Yanga.

Ushindi huo umeifanya Mwadui ipande hadi nafasi ya sita ikiwa na pointi 14 katika mechi nane.

Leave A Reply