The House of Favourite Newspapers

Yanga: Hatuwaachi Belouizdad Uwanja wa Mkapa Jijini Dar

0
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe.

UONGOZI wa Yanga hatima ya wao kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ipo mikononi mwa wapinzani wao CR Belouizdad ya nchini Algeria ambayo lazima wawafunge ili watimize malengo yao.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa marudiano wa hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa Jumamosi hii saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Timu hizo katika mchezo wa kwanza uliopigwa Algeria, Belouizdad walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0, na Jumamosi hii wanatarajiwa kuwepo uwanjani kupambana.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa mchezo huo ndiyo utaamua hatima yao ya kucheza kama watapata ushindi wa aina yoyote watakapokuwepo nyumbani.

Alisema kuwa kuelekea mchezo huo, hakuna kingine wanachokihitaji zaidi ya ushindi, ambao lazima waupate ili watimize malengo yao.

“Kuna nafasi kubwa ya Yanga kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika endapo tutashinda mchezo ujao dhidi ya CR Belouzidad.

“Na hakuna namna nyingine ya kufanya, hivyo ni lazima mchezo huo tutapate alama tatu hizo, kwenye kundi letu kila timu inaonesha kuwa ina uwezo wa kufuzu kwa lugha rahisi kila mtu ni mbabe.

“Kilichosaidia CR Belouizdad ni wingi wa mashabiki wao, ukweli ni kwamba sisi sio wanyonge kimsingi hatuwezi kufanikiwa bila uwepo wa mashabiki wetu ambao kwa dakika zote tuwe na sapoti kubwa, kuanzia dakika ya kwanza mpaka dakika ya mwisho, tusishangilie matokeo tunapaswa kushangilia kila dakika kuhakikisha mwarabu anapagawa.

“Jumamosi siyo mchezo wa kitoto, ni mechi ya kikubwa kweli. Benchi la ufundi kimsingi limejiandaa vya kutosha kwa upande wa mashabiki tunapaswa kufika na hasira ya kweli kila anayeamini analo jambo ambalo linaweza kusaidia timu yako kushinda basi lifanye,ruksa popote ulipo usimuogope mtu wewe fanya. Hakuna masihara mchezo ujao, tukitoka sare basi ujue tumeisha,” alisema Kamwe.

STORI: WILBERT MOLANDI

Leave A Reply