The House of Favourite Newspapers

Yanga hii, APR wapite wapi

0

Tambwe-Busungu-1 (1)Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema kuwa hatawafanyia utani wala kuwapuuza wapinzani wake katika Ligi ya Mabingwa Afrika, APR, badala yake atachezesha kikosi kamili lengo likiwa moja tu, kupata ushindi.

Yanga inakutana na APR katika mechi ya pili ya hatua ya kwanza ya michuano hiyo, kesho Jumamosi, baada ya ule wa kwanza Yanga kupata ushindi wa mabao 2-1, hali ambayo ilisababisha wengi kuamini kuwa mchezo huo wa pili utakuwa ‘mchekea’.

Mechi hiyo ya pili itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kocha huyo, ni wazi kuwa Yanga hawana utani hata kidogo.
Akizungumza na Championi Ijumaa katika mahojiano maalum, Pluijm alisema kikosi chake kipo fiti, kuna majeruhi kadhaa lakini hao siyo sababu ya wao kukosa ushindi.

“Nimeshawaambia wachezaji wote, hasa mabeki kuwa sitaki kusikia neno samahani, kwani kuna watu wamekuwa na kawaida ya kufanya makosa wanajua kuwa baadaye wataomba msamaha.

“Angalia mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal na Barcelona (juzi), ilikuwa na ushindani mzuri, Arsenal walikuwa wana nafasi ya kushinda lakini uzembe wa mabeki kuruhusu mabao ya kijinga na washambuliaji kushindwa kutumia nafasi, kumewafanya watolewe.

“Sitaki kuona kile kilichotokea hata katika mechi ya Juventus (juzi) ambayo walifungwa na Bayern mabao 4-2 kwa uzembe wao wenyewe.“Sisi tutaingia uwanjani kwa kazi moja tu ya ushindi, tutashambulia mwanzo mwisho.”

Wachezaji majeruhi
“Kwanza tutamkosa Juma Abdul ambaye ana kadi mbili za njano, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Makapu na Matheo Anthony ndiyo majeruhi.”

Tambwe: APR tutawakalisha
Straika wa Yanga, Amissi Tambwe, naye anafunguka: “Safari hii tumejipanga, tunataka kufika mbali, tumejipanga kushinda mechi zote za nyumbani na hata zile za ugenini pia, ndiyo maana nina uhakika mechi na APR tutapata ushindi.”

Niyonzima: Nikifunga nitashangilia
Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, hakuwa nyuma kuizungumzia mechi hiyo. “Nikifunga bao nitashangilia japokuwa najua APR kuna marafiki zangu na jamaa zangu wengi,” alisema Niyonzima ambaye ni mchezaji wa zamani wa APR.

Simba yatajwa kuhusika
Wakati presha kuelekea mchezo huo ikiwa kubwa, kuna taarifa kuwa mashabiki wa Simba wamehusika katika kuwakaribisha APR jijini Dar es Salaam kwa kuwatafutia hoteli iliyopo Msasani.
Habari ambazo zilifika mezani mwa Championi Ijumaa zilieza kuwa mashabiki hao wa Simba ndiyo waliowashawishi APR kufikia katika hoteli hiyo hata kabla hawajafika nchini wakati wakitambua kuwa hoteli hiyo imekuwa ikitumiwa na Yanga mara kwa mara.

Mtu wa karibu wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa uamuzi huo wa wapinzani wao ulifanyika kwa kuwa walijua hata waamuzi watafikishiwa kwenye hoteli hiyo lakini baada ya Yanga kupata taarifa hizo walibadili gia na kufanya maamuzi ya mabadiliko.

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema: “Tunakijua kila kitu kinachoendelea dhidi ya wapinzani wetu APR, tunajua wanashirikiana na moja ya klabu kubwa hapa nchini. Kama wao wanaendelea kuwasaidia waendelee tu, lakini watambue kuwa lazima tuwafunge APR.”

Leave A Reply