The House of Favourite Newspapers

Yanga Kukipiga na Polisi Tanzania Arusha leo, Watamba Kushinda

0

YANGA wanasema sasa zile dharau zimefika mwisho na leo wanarudi kwenye ubora wao wa kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara na vinara wa ligi hiyo, wamekuwa na mwendo wa kusuasua kwani katika mechi tano zilizopita baada ya kufanikiwa kushinda moja, sare tatu na kupoteza moja.

 

Leo Jumapili, Yanga watakuwa na wakati mwingine wa kurekebisha makosa yao pale watakapocheza dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

 

Wakati Yanga wakisema inatosha kudharauliwa, Polisi Tanzania nao wanasema inatosha sasa kushindwa kupata ushindi mbele ya Yanga.

 

Yanga iliyotoka kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union, tayari kocha wa kikosi hicho, Cedric Kaze amesema: “Mchezo uliopita haukuwa mzuri kwa upande wetu, hatukuwa vizuri karibia kila sehemu, yani hatukuwa bora katika mipira ya kugombea na kutengeneza nafasi.

Tumeyafanyia kazi yote hayo ili kuwa bora katika mchezo wetu dhidi ya Polisi Tanzania.“Muhimu kwetu katika mchezo huu ni kuona tunaibuka na ushindi na kuondoka na pointi tatu, wachezaji viongozi na mashabiki wote wanatamani kuona tunashinda, tutajitahidi ili kuendelea kuwapa furaha watu wote wa Yanga.

 

“Tupo katika mzunguko wa pili ambapo huwa mgumu kwa timu zote, timu nyingi hupambania malengo yao kwa kujitoa, hivyo hata Polisi Tanzania hawatakuwa tayari kupoteza mchezo huu, lakini tumejiandaa kupambana kwa ajili ya hilo.

“Niwaombe Wanayanga na wananchi wenzangu kuja kwa wingi uwanjani na kutupa sapoti kwa sababu tunaamini bila uwepo wao hali inakuwa ngumu kwa kiasi fulani.

 

Niwahakikishie tu kuwa hatutarudia makosa tena.”Polisi Tanzania ambayo ni wenyeji wa mchezo huo wa leo, wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kutoka kuichapa KMC bao 1-0 wakiwa hapo nyumbani.Rekodi za Yanga na Polisi Tanzania zinaonesha kwamba, timu hizo zimekutana mara tatu ndani ya Ligi Kuu Bara mpaka sasa.

 

Katika mechi hizo, Yanga imeshinda moja ile ya msimu huu kwa ushindi wa 1-0, huku mechi mbili za msimu uliopita zikiisha kwa sare. Ilikuwa 3-3 na 1-1.

 

Kutokana na kushindwa kupata ushindi mbele ya Yanga, Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amesema: “Wote tunajua Yanga ni timu kubwa na yenye wachezaji wazuri, hawajafanya vizuri kwenye mchezo uliopita, hivyo lazima wamekuja kwetu wakiwa wanataka alama tatu.

 

“Lakini haitakuwa rahisi kwa kuwa sisi tumejiandaa kuwakabili, kama walikosa pointi tatu msimu uliopita walipokuja kwetu, basi hata msimu huu mambo yatabaki kuwa vilevile.

 

Kwa kifupi tupo tayari kwa mchezo huo ambao tunataka kushinda.”Kabla ya mechi za jana Jumamosi, Yanga ilikuwa ikiongoza ligi hiyo ikikusanya pointi 49 baada ya kucheza mechi 22, imeshinda 14, sare saba na kupoteza moja. Polisi Tanzania ilikuwa ya nane na pointi zake 28 baada ya kucheza mechi 21, imeshinda sita, sare 10 na sare tano.

STORI: MARCO MZUMBE NA ISSA LIPONDA

Leave A Reply