The House of Favourite Newspapers

Zuchu Afanyiwa Dua Usiku na Baba Yake

0

SIKU zote damu ni nzito kuliko maji! Hicho ndicho kinachotokea kwa baba mzazi wa msanii mkali wa kike wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’, Othman Soud ambaye ameamua kujinyima usingizi na kumfanyia dua mwanaye huyo, Gazeti la IJUMAA linaripoti.

WAPO VIZURI…

Huko nyuma kulikuwa na madai mazito kwamba, baba huyo hakuwa na mawasiliano mazuri na mtoto wake huyo, jambo ambalo baba huyo aliliweka sawa na sasa hivi wapo vizuri.

Zuchu ambaye yupo chini ya lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB), ni uzao wa Mzee Othman Soud na Malkia wa Taarab Afrika Mashariki na Kati, Khadija Omari Kopa ‘Bi Khadija’.

 

IJUMAA NA BABA ZUCHU

Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na Gazeti la IJUMAA, baba wa Zuchu ambaye makazi yake ni Makadara visiwani Zanzibar, anafunguka namna ambavyo amekuwa akikesha kumuombea Zuchu kwa Allah amlinde na watu wabaya kisha azidi kuwa bora zaidi.

DUA NZITO USIKU MNENE

Baba wa Zuchu anasema kuwa, kila siku anamfanyia dua nzito mtoto wake huyo ili kumuepusha na mabaya kwa maana mafanikio ya Zuchu ni mafanikio yake pia.Baba huyo anazungumza kuhusiana na muziki anaofanya mtoto wake huyo pamoja na mafanikio mafupi aliyoyapata Zuchu ndani ya muda mfupi ambapo hajamaliza hata mwaka mmoja kwenye muziki;

 

IJUMAA: Habari za siku baba Zuchu? Mara ya mwisho kuwasiliana ulieleza namna ambavyo ulikuwa unasumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa kupooza kuanzia kiunoni mpaka chini, je, kwa sasa hali yako ikoje?

 

BABA ZUCHU: Asante kwa kunipa pole, kiukweli kwa sasa najisikia afadhali kidogo kwani ninaendelea vizuri sana. Angalau sasa ninaweza kutembea. Mwanzo nilikuwa sitembei kabisa wala kukaa, maana nilipooza kuanzia kiunoni kwenda chini.

IJUMAA: Pole sana, vipi Zuchu anakuja Zanzibar kukuona?

 

BABA ZUCHU: Ndiyo anakuja, juzi tu ametoka kuniona, kila anakuja kuniona.

 

IJUMAA: Unajisikiaje ukiona sasa wewe na mwanao mko vizuri na anakuja kukuona kama hivi unaumwa?BABA

ZUCHU: Ninajisikia vizuri sana, damu ni nzito kuliko maji na ninafurahi mno, maana yule ni mtoto wangu na ninampenda sana.

 

IJUMAA: Unajisikiaje kuhusiana na kazi yake ya muziki anayofanya kwa sasa na kuwa msanii bora wa kike nchini?

BABA ZUCHU: Ninajisikia vizuri sana, lakini ninachokifanya huwa ninaamka usiku mnene na kumfanyia dua siku zote. Kwa kufanya hivyo naamini anakuwa salama dhidi ya watu wabaya dhidi yake na atazidi kuwa bora zaidi kwenye sanaa yake ya muziki.

 

IJUMAA: Je, katika watoto wako, kuna mwingine ambaye anaimba au amefuata nyayo zako kwenye sanaa kama ilivyo kwa Zuchu?

 

BABA ZUCHU: Hakuna mtoto mwingine aliyefuata nyayo zangu zaidi yake na ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili yake na namna anavyomjaalia mafanikio.

 

IJUMAA: Umekuwa baba wa tofauti sana ukilinganisha na wazazi wa wasanii wengine ambao ni mastaa wakubwa nchini; maana watu wengi hawakufahamu, je, ni kwa nini?

BABA ZUCHU: Mimi kwa kweli tangu zamani huwa sipendi mambo ya mitandao ya kijamii na kusema kweli sijui lolote kuhusu mitandao, hivyo siwezi kuja kuonekana hovyohovyo mitandaoni.

IJUMAA: Kuhusu ugonjwa wa kuooza umeshapata ufumbuzi au matibabu kamili?

BABA ZUCHU: Nimepata ufumbuzi ndiyo ninafanya matibabu na sasa ni afadhali sana kwani natembea, tofauti na mwanzo ambapo hata kukaa nilikuwa siwezi kabisa.

IJUMAA: Polesana baba Zuchu na ugua pole.

BABA ZUCHU: Asante sana, karibu tena.

TUJIKUMBUSHEKabla ya baba Zuchu kuibuliwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers, kulikuwa na maswali ya watu wengi kutaka kujua mahali alipo mzazi huyo ambapo pia yalizungumzwa mengi kwenye mitandao ya kijamii.

Kuna ambao walisema Zuchu na baba yake huyo wana ugomvi mzito, lakini hata hivyo, baada ya gazeti hili kuandika habari ya mzazi huyo kwa mara ya kwanza, Zuchu alifika visiwani Zanzibar na kukutana na mzazi wake hiyo kisha akashea picha ya pamoja kupitia ukurasa wake wa Instagram na sasa wapo vizuri mno.

Stori:IMELDA MTEMA, Dar

MJAMZITO ALIA – “ASKOFU Aliniahidi KUNIOA na KULEA MIMBA YANGU, KAKIMBIA SIKU 2 KABLA YA NDOA YETU”

Leave A Reply