The House of Favourite Newspapers

Yanga: Ubingwa Kwetu ni Mubashara

STORI: Said Ally na Khadija Mngwai| CHAMPIONI

YANGA inaongoza Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi moja, leo Ijumaa itakuwa uwanjani kukipiga dhidi ya Stand United na jambo pekee ambalo timu hiyo ya Jangwani imesisitiza ni kuwa inachohitaji ni kupata ushindi ‘live’ bila longolongo, yaani kwa lugha ya kisasa unaweza kuuita ushindi mubashara.

Yanga inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 46, wakati kabla ya mechi za jana, Stand ilikuwa nafasi ya sita ikiwa na pointi 26, ushindi kwa Yanga leo utaifanya timu hiyo kujiimarisha kileleni na kutengeneza mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wakati Stand ikishinda inaweza kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupanda katika nafasi za juu.

Kikosi cha Yanga

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, aliliambia gazeti hili kuwa wanataka kushinda mechi hiyo kwa sababu kuu mbili, kulipa kisasi na kuongeza wigo wa pointi na wapinzani wao ili wasishuke kileleni kwa kuwa hawataki hilo litokee.

“Stand wao mechi ya kwanza walitufunga lakini safari hii hatutaki hilo litokee na tunataka kulipa kisasi, hivyo wajiandae kwa kupoteza mechi.

“Tunataka kushinda kwa sababu ya kuongeza wigo pointi baina yetu na wanaotufuatia, hivyo tutacheza kwa jihadi ilimradi tupate pointi zote tatu,” alisema Mwambusi na kuongeza:

“Maandalizi yanaendelea vizuri kabisa, kikubwa tunashukuru, majeruhi yupo mmoja ambaye ni Busungu (Malimi) mwenye majeraha ya enka.

“Habari njema ni kuwa, beki wetu Dante (Andrew Vicent) amepona enka na amerejea uwanjani baada ya kuikosa mechi iliyopita dhidi ya Mwadui.

“Hivyo, kesho huenda akawepo uwanjani mechi na Stand United baada ya kuwa fiti kwa asilimia kubwa, ni baada ya daktari kumfanyia vipimo.

“Tunataka tuendelee kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi, ni baada ya kuwaondoa Simba kileleni,” alisema.

Aidha, Daktari wa Yanga, Edward Bavo alisema mshambulaiji wao Donald Ngoma alifanya mazoezoi pamoja na wenzake baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akiwa majeruhi, ambapo amesema kama kocha akiamua kumpanga hakuna tatizo.

Upande wa Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema: “Kikosi chetu kipo vizuri, tunakijua vizuri kikosi cha Yanga pamoja na safu yake ya ushambuliaji, hata katika mzunguko wa kwanza tuliwafunga.”

Championi Ijumaa, Toleo la Februari 3, 2017

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Save

Comments are closed.