The House of Favourite Newspapers

Ni Udhamini wa Azam TV Ndio Unaifanya TFF Kuwa Laini kwa Azam Fc?

Kikosi cha Azam FC

MAKALA: Na Saleh Ally | CHAMPIONI

NDANDA FC wamesema wanaendelea kusafiri kutoka Mt­wara kuja Dar es Sa­laam kwa ajili ya ku­wavaa Azam FC katika mechi yao iliyopangwa kuchezwa kesho Ju­mamosi.

Lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema limei­sogeza mechi hiyo hadi Februari 7 ili kuipa nafasi Azam FC kucheza mechi yake ya kirafiki ya kimatai­fa dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Mamelodi ni mab­ingwa wa Afrika, wa­likuja nchini kwa ajili ya kucheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Sim­ba, Yanga na baadaye Azam FC, vigogo hao wawili wakagoma na kuonyesha wanajitam­bua.

Azam Fc wakishangilia

Mwisho Azam FC wakakubali kucheza mechi hiyo ya kirafiki na kufanikiwa kutoka 0-0 dhidi ya mabingwa hao. Mechi ambayo ilihud­huriwa na mashabiki ambao hata 200 hawakufika!

Kocha Pitso Mosi­mane wa Mamelodi ni rafiki yangu kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Urafiki wetu ulianza baada ya yeye kumchukua Selemani Matola wa Simba kwenda ku­jiunga na kikosi cha Super­Sport United cha Afrika Kusini baada ya mi­chuano ya Tusker jijini Nairobi, Kenya.

Mosimane alini­ambia wanajiandaa na mechi kadhaa ikiwemo dhidi ya Kaizer Chiefs tare­he 8. Alinieleza wamekuja huku baada ya kuwa wako ‘free’ na ha­wana michezo inayowabana na walitaka sana kucheza na vigogo hasa Simba ambayo wanaamini in­aongoza kwa makombe mengi kwa rekodi wali­zonazo.

Wao wamekuja huku kwa kuwa ratiba ina­waruhusu na hakuna sehemu ambayo wa­navuruga ratiba ya ligi. Mechi zao hapa zilitakiwa kuvuruga ratiba ya ligi na mwisho imekuwa hivyo.

Jamali Malinzi.

Kama Yanga na Simba wangekubali kucheza nao, basi huenda ratiba inge­vurugika zaidi. Unaona wakati Yanga wanakuwa wa kwanza kukataa na un­agundua waliona jambo sahihi, kwani hakuna fa­ida ya kucheza na Mame­lodi kipindi hiki katikati ya ligi.

Awali, tulielezwa Sim­ba walikuwa wamekubali wacheze juzi Jumatano, lakini nao wakakataa huenda baada ya kujitathmini au waliona namna ambavyo Yanga walifanya ambalo lilikuwa jambo sahihi. Sijui kama wao wangeku­bali kucheza, TFF ingesogeza mbele michezo yao?

Azam wamekubali na TFF im­esogeza mchezo huo mbele bila ya kujali mipango ya Ndanda FC iko­je. Lazima tukubali kwamba, haki kama unazungumzia katiba au ka­nuni za uendeshaji ligi kuu, Ndan­da FC wana haki na hadhi sawa na Azam FC, kwa kuwa zote ni timu za ligi kuu.

Hakuna kigezo kwa mujibu wa kanuni au sheria yoyote inayoweza kuipa Azam FC ubora au ukubwa zaidi ya Ndanda FC. Kama ni hivyo, basi TFF inapaswa kuziheshimu timu zote za ligi kuu na kuachana na woga usiokuwa na sababu za msingi.

Msimu uliopita, TFF ilikubali kuvuruga ratiba ya ligi kuu, ika­wapa nafasi Azam FC kusafiri hadi Zambia kushiriki tamasha la timu kadhaa. Wakati tamasha hilo lina­fanyika Zambia, ligi yao ilikuwa imesimama kwa kuwa wanaelewa ukubwa na thamani.

Walisema lengo ni kusaidia kuii­marisha Azam FC wakati wa ushiriki wa kimataifa. Ilifikia wapi? Wote tu­najua na msisitizo tokea huo msimu uliopita nilieleza namna TFF inavy­oshindwa hata kuthamini kinach­oiweka mjini. Bila ligi kuu yenyewe itatambulika wapi, itakuwa inafan­ya nini? Viongozi wake kwa nini wa­nashindwa kulielewa hili na kuona tamasha ni bora kuliko ligi?

Leo wamefikia wanaona mechi ya kirafiki, eti kisa ni mabingwa Af­rika, ni bora kuliko ligi kuu? Hawa vi­ongozi ni wa namna gani au ulaini na woga wao kwa Azam FC ni upi?

Wasitake watu tuanze kuamini kupitia ujumlisho wa mambo, kwamba kwa kuwa wanadhamini­wa na Azam TV ambayo pia inami­likiwa na makampuni ya Bakhresa ambao ni wadhamini wa michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa na maana ni wadhamini wa TFF, basi wanashindwa kuwa huru au kuwa na maamuzi sahihi linapofikia sua­la la Azam FC!

Hii si sahihi, misimu miwili mfu­lulizo TFF inaonekana kujilainisha katika masuala yanayoihusu Azam bila ya kuangalia haki ya timu ny­ingine zinazoshiriki ligi.

Mimi naiunga mkono na kui­pongeza Azam TV kwa udhamini wa michuano ya Kombe la Shirik­isho na niseme wanapaswa ku­ungwa mkono kwa kuwa wame­ingiza fedha nyingi sana, tena ni chombo cha habari.

Niwe wazi, kamwe hata kidogo bila ya woga siungi mkono tabia za kizabizabina za TFF kama wanazoz­ifanya ambazo zinaonyesha wazi ni waoga, wasio na maamuzi sahihi na huenda wanataka kuwafurahi­sha wadhamini kwa njia nyingine ambazo si sahihi.

Mwisho wito wangu kwa TFF, wao ndiyo wanatakiwa kuwa watu wa kwanza kuonyesha heshima ya juu kwa ligi kuu na timu zina­zoshiriki na wajue, kama hakuna timu za ligi kuu na ligi nyingine, TFF haitakuwepo na wala haitakuwa na fedha za kuingiza kwa kuwa haina hata duka la kuuza mafuta ya taa!

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Comments are closed.