Yanga waenda kuutema ubingwa Kirumba

YANGA wamemaliza mechi zao za Dar es Salaam na sasa wamehama makazi yao na kuelekea mkoani Mwanza katika Uwanja wa Kirumba. Lakini kuelekea huko kunaweza kukawa kuchungu kwao kiasi cha kushindwa kutwaa ubingwa kwa msimu huu kutokana na ‘gundu’ walilonalo katika uwanja huo.

 

Yanga wamelazimika kuondoka Dar na kwenda Mwanza kutokana na kufungwa kwa Uwanja wa Taifa ambao umepigwa pini kwa ajili ya marekebisho ya kuuandaa kutumika Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17.

 

Klabu hiyo yenye pointi 67 hadi sasa, awali kabla ya kuuchagua Kirumba walikuwa wanapiga hesabu za kwenda Samora, Iringa lakini mwisho wakaupendekeza Kirumba.

 

Licha ya kuhamia hapo Kirumba, uwanja huo siyo rafiki kwao kutokana na rekodi isiyo nzuri katika mechi za karibuni. Awali, Yanga ilikuwa ina uhakika mkubwa wa kushinda ndani ya uwanja huo wakati Toto Africans ilipokuwepo ambapo misimu ya 2015/16 na ule wa 2016/17 walikomba pointi zote sita, lakini baada ya kuja kwa Mbao mambo yamebadilika.

 

Katika misimu miwili iliyopita mambo yalikuwa mabaya kwa Yanga baada ya kuangusha pointi sita wakifungwa na Mbao kabla ya msimu huu kuamka. Yanga walipoteza mechi zao hapo kwa vipigo vya 2-0 msimu wa 2017/18 na kile cha 1-0 msimu wa 2016/17, wenyewe wameshinda msimu huu kwa mabao 2-1.

 

Lakini pia uwanjani hapo, Yanga kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Merreikh ya Sudan, walilazimishwa suluhu kabla ya kufungwa Sudan mabao 2-0 na kutupwa nje.

 

Hii ina maana kwamba Yanga baada ya kuuchagua uwanja huu wa Kirumba, wanatakiwa wawe makini la sivyo mambo yanaweza kuwabadilikia. Kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera akizungumzia juu ya kuhamia uwanja huo. Amesema: “Hakuna tatizo kuja uwanja huu, tunajiandaa kufanya vizuri hapa kama ilivyokuwa Uwanja wa Taifa.”

Toa comment