The House of Favourite Newspapers

Yanga wamkomalia Mo… Waapa kumchomoa Mkude Simba SC

SAKATA la usajili wa kiungo wa Simba, Jonas Mkude ambaye anamaliza mkataba wake na klabu hiyo hivi karibuni limeendelea kupamba moto na uongozi wa Yanga umedai kuwa unaendelea kupambana kuhakikisha unamchomoa mchezaji huyo klabuni hapo.

 

Unaambiwa kuwa licha ya hivi karibuni Mwekezaji Mkuu wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kuwataka Wanasimba kutokuwa na wasiwasi kuwa Mkude haendi popote baada ya kufanya naye mazungumzo mara tu aliposikia kuwa timu hiyo imemtengea Sh milioni 120, mambo bado ni moto.

 

Habari za kuaminika ambazo Championi Jumatatu limezipata kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa uongozi wa timu hiyo bado unaendelea kupambana na Mo ili kuhakikisha unamchomoa Mkude katika kikosi hicho cha Simba ambacho ameanza kukitumikia tangu msimu wa 2011/12 baada ya kupandishwa kutoka kikosi cha vijana.

 

“Bado tunaendelea kupambana ili kuhakikisha tunamsajili Mkude kutoka Simba kwani licha ya kukutana na Mo hivi karibuni bado mambo kwa upande huo hayajakaa sawa.

“Fedha ambayo Mo anataka kumpatia haina tofauti kubwa na ile waliyompatia miaka miwili iliyopita wakati alipokuwa akisaini mkataba ambao unamalizika hivi karibuni na inavyoonekana hawapo tayari kumwongezea.

 

“Kwa hiyo, baada ya kuona hivyo tuliamua kumtafuta meneja wake ambaye pia ni mwanasheria wake na kuzungumza naye na bila kusita ametuambia kuwa kama kweli tunamtaka basi tutoe Sh milioni 120 sababu Simba fedha wanayotaka kumpatia ni kidogo,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Meneja wa Mkude ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini, alisema: “Ni kweli kabisa ishu ya Mkude kuongeza mkataba mpya na Simba bado mambo hayajakaa sawa, kwani fedha wanayotaka kumpatia haina tofauti na ile ya miaka miwili iliyopita.

 

“Lakini pia Yanga bado nao tunaendelea kuzungumza nao, ila wao ofa yao kidogo ipo juu, ni nzuri, lakini nimewaambia waongeze kama kweli wanamtaka watoe Sh 120 milioni ambayo walikuwa wamemuahidi. Miaka yake nayo inazidi kwenda kwa hiyo hawezi kubaki Simba kwa sababu anaipenda tu huku akipata maslahi kidogo na kuacha kwenda kujiunga na timu ambayo imetoa fedha nyingi ambazo zitamwezesha kuitengeneza vizuri kesho yake.”

 

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

Comments are closed.