The House of Favourite Newspapers

Yanga Wanaishi Kishua Waboresha Mishahara ya Wachezaji, Lengo

0
NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga.

UKISEMA fedha inaongea, hutakosea kwani mabosi wa Yanga wameamua kuweka mikakati mizito kuhakikisha nyota wa kikosi hicho wanaishi kishua kwa kuboresha mishahara ya wachezaji, lengo likiwa ni vijana hao kutimiza majukumu yao ya uwanjani kuanzia michuano ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa timu hiyo uingie mkataba wa miaka mitano na GSM Company Group wenye thamani ya Sh 9.1Bil na ule wa GSM Foam wenye Sh 300Mil, ambapo kutakuwa na ongezeko la asilimia 10 kila mwaka hadi kufikia jumla ya shilingi bilioni 10.9.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema katika kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri ya ushindi, haraka wametoa kipaumbele maboresho ya mishahara ya wachezaji kwa kutofautisha matumizi yatakayotokana na mapato kutoka kwenye udhamini.

Mayele na Aziz Ki wakifanya yao mazoezini.

Hersi alisema mapato yatakayotokana na udhamini kutoka GSM Foam zenyewe zitakwenda moja kwa moja katika malipo ya mishahara ya wachezaji pamoja na yale wanayoyapata kutoka makampuni mengine ya Taifa Gas, SportPesa, Afya Water, Azam Media na mengineyo.

 

Aliongeza kuwa, fedha zitakazotokana na utengenezaji wa jezi na vifaa vingine vya michezo vinayotengeneza na GSM Group Company ambazo ni shilingi bilioni 9.1, zitakwenda katika ujenzi wa uwanja wao mpya huko Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 

“Hatutaki kusikia wachezaji wetu wakilalamikia mishahara, kwani ili timu ifanye vizuri ni lazima walipwe kwa wakati pamoja na kuboresha mishahara hiyo.

 

“Hivyo mkataba wa Sh 300Mil ambao kila mwaka kutakuwepo na ongezeko la asilimia kumi tutazozipata kutoka GSM Foam sambamba na zile fedha za udhamini wa makampuni mengine, moja kwa moja zitakwenda katika mishahara kwa kuhakikisha tunawaboreshea wachezaji wetu na benchi la ufundi.

 

“Pia zile tutakazopata kutoka GSM Company Group ambazo ni shilingi bilioni 9.1 zitakazotokana na utengenezaji na mauzo ya vifaa vya michezo, zitakwenda katika ujenzi wa uwanja pekee,” alisema Hersi.

WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

Leave A Reply