The House of Favourite Newspapers

Yanga Yafyatua Mitego Sudan, Yabadili Siku ya Kuwafuata Al Hilal, Injinia Afunguka!

0

RAIS wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo, kwa kuwaambia kwamba wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupangua fitina na hujuma zote ugenini wakisaidiwa na Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Silima Haji Kombo ambaye ndiye atakuwa mwenyeji wao.

 

Hiyo ni katika kuhakikisha wanawafunga wapinzani wao Al Hilal katika mchezo wa marudiano wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utapigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Al Hilal uliopo Sudan.

 

Yanga katika mchezo huo, wanahitaji ushindi wowote ili wafanikiwe kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, kutoka sare ya bao 1-1.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Hersi aliwahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa, kikosi chao kitaenda Sudan Jumamosi alfajiri na sio leo Alhamisi kama walivyopanga awali kwa kuhofia hujuma zitakazotokana na Uviko-19 ambazo wachezaji wao watapewa.

Hersi alisema mara baada ya kikosi hicho kutua Sudan, kitapokewa na Balozi wa Tanzania nchini humo ambapo jioni watapata chakula cha pamoja nyumbani kwake kabla ya usiku saa tatu kamili kuongozana naye kwenda katika mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo utakaopigwa kesho yake Jumapili.

 

“Tumepata msaada mkubwa sana kutoka kwa balozi wetu ambaye yupo nchini Sudan, kuelekea mchezo huu wa marudiano ambaye yeye tutakuwa naye kwa kipindi chote, timu itafikia nyumbani kwake mara baada ya kutua hapo.

 

“Mashindano haya ya Afrika yamekuwa magumu sana haswa kwa mechi za ugenini, lakini sisi kama viongozi tumeamua kupunguza siku za kukaa kule Sudan ili kupangua hujuma mbalimbali ambazo wenyeji wetu wanaweza kuzifanya.

 

“Napenda niwahakikishie mashabiki wote wa Yanga kuelekea mchezo huu, tumejipanga vizuri sana kuwakabili wenyeji wetu huko kwako.

 

“Tuna wachezaji wengi wazuri na wakubwa ambao washacheza michezo kama hii, hivyo tumejiandaa vizuri, kilichotokea hapa nyumbani Dare es Salaam ni sehemu ya matokeo tu, bado tuna nafasi nyingine ya dakika 90 pale Sudan,” alisema Hersi na kuongeza kuwa:

 

“Naomba niwahakikishie mashabiki wetu na wanachama wote wa Yanga kuwa, kocha wetu Nabi bado ana mkataba na sisi na hatujampa mechi mbili wala moja, sisi kama uongozi hatufanyi kazi kwa mihemko ya watu.

 

“Nabi ni kocha wetu na ndiye mwenye dhamana kubwa ya kuamua nini tufanye kwenye timu kwa sasa.”

 

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Saad Kawemba, alisema safari ya kuwafuata wenyeji wao Al Hilal ni Jumamosi na Ndege ya Shirika la Ethiopia.

 

Msafara huo wa Yanga utakuwa na jumla ya wachezaji 25, benchi la ufundi lenye watu 11 pamoja na viongozi na mashabiki.

 

“Yanga itaanza safari Jumamosi jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10:00 alfajiri na Ethiopian AirWays, tutatua Sudan saa 6:40 mchana ambayo ni sawa na majira ya 5:40 asubuhi kwa hapa Tanzania.

 

“Baada ya kutua nchini hapo, kikosi chetu kitapumzika hadi majira ya saa 2:00 usiku sawa na 3:00 usiku kwa hapa Tanzania na tutafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Al hilal ambao utatumika kwenye mchezo wa marudiano,” alisema Kawemba.

 

Katika hatua nyingine, Yanga imepanga kutumia jezi mpya walizozitambulisha juzi ambazo zimetengenezwa maalum kwa ajili ya kumuenzi Hayati Julius Kambarage Nyerere, watakapoikabili Al Hilal.

STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

CHEKI WACHEZAJI WA SIMBA WAKIPASHA TAYARI KUWAVAA DE AGOSTO JUMAPILI KWA MKAPA..

Leave A Reply