The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaleta Beki Mnigeria Usiku Mnene

0
Mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma.

HENRY Tony Okoh ni yule beki raia wa Nigeria ambaye tulimtaja jana kwenye Championi Ijumaa kwamba Yanga imepanga kumsajili ili kuziba pengo la Vincent Bossou. Kwa taarifa yako beki huyo tayari ametua nchini usiku wa saa 9 kuamkia jana Ijumaa, imethibitishwa.

Yanga imepanga kumpa mkataba wa miaka miwili beki huyo ili achukue nafasi ya Bossou ambaye amemaliza mkataba na hatoweza tena kuongezewa mkataba. Timu hiyo, tayari imefanikiwa kunasa saini za nyota wanne ambao ni kipa Rostand Youthe, Pius Busitwa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Donald Ngoma wote wakisaini mikataba ya miaka miwili. Ngoma ameongeza mkataba. Kwa mujibu wa bosi mmoja wa Yanga mwenye sauti kwenye Kamati ya Usajili, beki huyo ambaye msimu wa 2015/16 alichezea Akwa FC alitua nchini kwa ndege ya Rwanda Airways na kupokelewa na viongozi wa kamati hiyo.

Ngoma na Kamusoko wakishangilia katika moja mechi za Ligi Kuu Bara msimu 2016/7.

Mtoa taarifa huyo alisema, beki baada ya kuwasili alipelekwa kwenye moja ya hoteli kubwa hapa nchini kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya mwisho kabla ya kumpa mkataba wa kusaini. Aliongeza kuwa, Mnigeria huyo muda wowote atasaini mkataba wa miaka miwili na inaelezwa anachukua nafasi ya Mzambia, Justine Zulu atakayesitishiwa mkataba wake.

“Kama tulivyotangaza awali kwenye usajili wetu, tumepanga kuufanya kimyakimya na leo (jana) saa tisa alfajiri tumemshusha beki mwingine wa kati mwenye uwezo mkubwa. “Hivi sasa hatuangalii ubingwa wa ndani kwa maana ya ligi kuu ambao tumeuchukua mara tatu mfululizo, hivyo basi nguvu zetu tunazielekeza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Na tumemleta Mnigeria huyo baada ya kupokea ripoti ya kocha ikimuhitaji beki mmoja wa kimataifa mwenye uwezo na uzoefu mkubwa ndani ya uwanjani, hivi ninavyoongea na wewe yupo hotelini amepumzika huku tukimalizana baadhi ya vitu kabla ya kusaini,” alisema mtoa taarifa huyo. Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alizungumza suala hilo na kusema kuwa “Suala la usajili anayetakiwa kulizungumza hivi sasa ni mwenyekiti wa kamati ya usajili ambaye ni Nyika (Husseni) na siyo mimi.” Alipotafutwa Nyika kuzungumzia hilo kwa njia simu alipokea na kujibu kifupi tu: “Nipo kwenye kikao nipigie baadaye.” Hata baadaye jioni alipotafutwa tukielekea mitamboni alisisitiza bado yupo kikaoni

Leave A Reply