The House of Favourite Newspapers

YONDANI APEWA RUNGU YANGA

 

BENCHI la ufundi la Yanga, chini ya Kocha Mwinyi Zahera limempa mamlaka beki Kelvin Yondani kuwa mchezaji kiongozi ndani ya kikosi hicho akisaidiwa na Juma Abdul ambaye ni swahiba yake mkubwa na ambaye hata kwenye usajili walitikisa.

 

Yondani ambaye alifanya vizuri na Yanga msimu uliopita anapewa nafasi aliyokuwa akiikaimu msimu uliopita baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kupoteza namba yake kwenye kikosi cha kwanza.

Siyo hilo tu, Zahera amebainisha kwamba siku si nyingi atatua Kocha Mzanzibari kwenye kambi yao iliyopo Morogoro ambaye jukumu lake itakuwa kunoa makipa wa Yanga na Noel Mwandila atafanya kazi ya kuwaweka fiti kwenye idara ya viungo.

 

Spoti Xtra linajua kwamba kuna viongozi wa Yanga, wanamtaka Kocha Mecky Maxime wa Kagera kuwa msaidizi wa Zahera lakini Mkongomani huyo mwenye uraia wa Ufaransa anasema hajasikia lolote na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuchagua nani wa kufanya nae kazi.

 

Kikosi cha Yanga kwa sasa kipo mkoani Morogoro kikiendelea na maandalizi yake ya msimu mpya pamoja na kukamilisha ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Zahera ambaye anazungumza Kiswahili cha lafudhi ya Kikongo anasema ; “Nimefanya uchaguzi wa nahodha wa timu juzi Ijumaa na Kelvin Yondani alipewa hiyo nafasi, atasaidiana na mwenzake Juma Abdul kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa.”

 

“Kwa hiyo hawa watafanya kazi na wenzao kuhahikisha mambo yanakwenda sawa hasa suala la nidhamu linakuwa vizuri ndani ya kikosi chetu ambacho kwa sasa tunapambana kuhakikisha timu inakuwa sawa,” anasema Zahera ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo.

 

Kocha huyo anasema amefanya uteuzi wa wachezaji hao kwa kuzingatia uzoefu wao, uwezo wao ndani na nje ya uwanja, ushawishi wao kwa wenzao pamoja na ukongwe ndani ya timu na anaamini kwamba wataiongoza vyema Yanga ndani haswa ndani ya Uwanja.

 

KOCHA MZENJI

Zahera ingawa hakutaja jina lakini ameiambia Spoti Xtra jana kwamba ana mpango wa kuleta msaidizi wake kutoka DR Congo lakini kocha wa makipa viongozi wamemwambia atatoka Zanzibar wala siyo Kenya.

 

Mzanzibari huyo ambaye wanamfanya siri atakuja kuchukua nafasi ya Juma Pondamali aliyekaa pembeni kwa sababu za kimasilahi. Kocha Mkenya Razack Siwa alionekana Jangwani hivi karibuni lakini habari za ndani zinasema wameamua kumpiga chini kimyakimya.

 

ATULIZA MASHABIKI

Zahera anasema kwenye kambi ya Morogoro wanafanya mazoezi ya ukweli kusaka ufiti kwa wachezaji baada ya kugundua kwamba hali si nzuri lakini amewataka mashabiki kutokuwa na wasiwasi sana.

 

Kocha huyo anaamini kwamba kwa aina ya timu aliyonayo licha ya kwamba si asilimia 100 ya kile alichotaka lakini inaweza kufanya vizuri kwenye mashindano anayoshiriki ambayo ni ligi ya ndani na Kombe la FA.

 

Yanga na Simba zinatarajia kucheza Septemba 30, mwaka huu katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi ambayo inaanza Agosti 22.

 

“Wachezaji wanavyokuja ndivyo wanavyoendelea na mazoezi kwa sababu ukiangalia wale ambao walikuwepo wakati tunaanza wapo vizuri licha ya kwamba hawajafikia utimamu wa asilimia mia tofauti wale ambao wanakuja sasa hivi ambao wanahitaji zaidi ya wiki tatu mpaka nne ili kuweza kuwa sawa.

 

“Haitochukua muda naamini timu yangu itakuwa imekamilika kwa asilimia zote baada wakati huo kwa kuwa timu imeshakamilika na itakuwa na uwezo wa kufanya chochote ambacho kitawashangaza watu na hata hawatoamini kitu ambacho kitatokea kwenye mchezo wa siku hiyo kwa sababu tutakuwa tumeshakuwa sawa kwa kila kitu.”

 

“Sasa kabla ya ligi kuanza ni lazima tufanye bidii kwa ajili ya kuongeza ufiti wao kabla ya kuanza kupambana na wenzetu. Kama tukishindwa kuwa na levo moja inayofanana basi tutakuwa na wakati mgumu sana mbele,” anaongeza Zahera na kusisitiza kwamba mpaka mechi ya Simba ifike watakuwa fiti.

 

MAJUKUMU MUHIMU YA YONDANI

Miongoni mwa majukumu ya Yondani sasa kama nahodha ni kujenga umoja ndani ya wachezaji wa Yanga, kufanya kazi kwa mfano ndani na nje ya uwanja, kujadili na kocha kuhusiana na mambo muhimu pamoja na kutoa maoni kwenye upangaji wa kikosi.

 

Mbali na hilo pia Yondani anatakiwa kujiamini zaidi ya wachezaji wenzake, kufanya maamuzi kwa akili ndani ya uwanja, kujua ubora na udhaifu wa kila mchezaji ndani na nje ya uwanja pamoja na kuwajengea morali ya kupambana katika mazingira yote.

 

Yondani pia anapaswa kuwasiliana kwa nguvu ndani ya uwanja kwa chochote kile kinachotokea na pia kujua kinachoendelea ndani ya timu na kuzungumza na wenzie na hatakiwi kuwa mtu wa kupaniki.

STORI: MARTHA MBOMA NA IBRAHIM MUSSA

Comments are closed.