The House of Favourite Newspapers

Yondani, Kakolanya wafungiwa

HALI ya mambo ndani ya Yanga sasa si shwari tena kwani muda wowote kuanzia leo kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya anaweza kuvunja mkataba. Lakini yeye pamoja na Kevin Yondani wameshafungiwa.

Hali hiyo inatokana na uongozi wa Yanga kushindwa kufikia mua­faka na kipa huyo juu ya madai yake ikiwa ni pamoja na malipo ya mshahara wake wa miezi minne.

 

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Kakolanya pamoja na nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani, waligoma kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya mechi za Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui FC na Kagera Sugar, la­kini pia baada ya timu kurudi Dar es Salaam, bado wachezaji hao wameendelea kuwa nje ya kikosi hicho wakitaka walipwe stahiki zao wanazodai.

Meneja wa Kakolanya, Selem­ani Haroub, alisema kuwa mpaka kufikia jana, kipa huyo na uongozi wa Yanga walikuwa bado hawa­jafikia muafaka juu ya jambo hilo kutokana na uongozi huo ku­toonyesha ushirikiano.

 

“Tumekuwa tukiwatafuta vi­ongozi wa Yanga na hasa katibu mkuu ili kuzungumzia suala hili lakini wamekuwa hawaonyeshi ushirikiano, kwa hiyo kesho (leo) ndiyo mwisho, baada ya hapo tu­tajua nini cha kufanya,” alisema Haroub.

Alipoulizwa Kakolanya kuhusi­ana na hilo, alisema: “Katika hili siwezi kusema lolote ila meneja wangu ndiye anayejua kuwa wamefikia wapi uongozi wangu. Ila ni kweli kuna mambo ambayo ndiyo yamesababisha nisiwe na timu mpaka sasa.”

 

Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya, alipotafutwa jana, alikuwa akikata simu mara kwa mara, huku Meneja wa Yanga, Nadir Ha­roub akisisitiza kuwa anachofa­hamu Beno bado ni mchezaji wa Yanga.

Katika hatua nyingine, kocha Mwinyi Zahera, amewafungia mechi mbili, Yondani na Ka­kolanya kutokana na kudaiwa kugomea kuichezea timu hiyo wakidai fedha za mshahara.

 

Chanzo cha kuaminika kuto­ka ndani ya Yanga kimeliambia Championi Jumatatu, kwamba Zahera hana mpango kabisa wa kuwatumia wachezaji hao katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons (leo Jumatatu) sam­bamba na mchezo unaokuja dhidi ya Biashara United.

“Yeye kaona kwamba bora aendelee na wachezaji wach­ache ambao watakuwa na moyo wa kuitumikia timu to­fauti na wale ambao wanago­ma,” kilisema chanzo hicho.

SWEETBERTLUKONGE NA SAID ALLY

Comments are closed.