The House of Favourite Newspapers

Zahera Aanza Kazi Yanga, Kusafiri na Timu Nigeria

0

UONGOZI wa Yanga umepanga kumtambulisha rasmi Mwinyi Zahera kuwa Mkurugenzi wa Soka la Vijana ndani ya klabu hiyo huku akiwa na uwezo wa kutoa ushauri kwa timu kubwa lakini kubwa kuliko ni kusafiri na timu hiyo kuelekea nchini Nigeria kwa ajili ya kutoa msaada kwa benchi la ufundi.

 

Yanga Ijumaa hii inatarajiwa kusafiri kwenda nchini Nigeria kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ambao utapigwa Septemba 19.

 

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini hapa Jumapili iliyopita, Yanga ilikubali kichapo cha bao 1-0 hivyo sasa wanatakiwa kushinda kuanzia mabao 2-0 ili wasonge mbele moja kwa moja.

 

Baada ya mchezo huo kumalizika, Yanga itarejea kujiandaa na mchezo mwingine mgumu dhidi ya watani zao, Simba utakaopigwa Septemba 25 ukiwa ni wa Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Mkapa mkoani Dar.

 

Chanzo chetu cha uhakika kutoka Yanga kimeliambia Championi Jumatano kuwa, uongozi wa Yanga wiki hii unatarajiwa kumtambulisha Zahera kama mkurugenzi wa maendeleo ya soka la vijana la klabu hiyo na baada ya hapo uongozi umepanga kumuongeza Zahera katika safari ya kwenda Nigeria kwa ajili ya kuongeza nguvu katika mchezo huo wa ugenini.

 

“Uongozi wa Yanga wiki hii unatarajiwa kumtambulisha kocha Zahera kuwa mkurugenzi wa maendeleo ya soka la vijana ndani ya Yanga na baada ya hapo uongozi huo umepanga kocha huyo kusafiri kwenda Nigeria kwa ajili ya kuongeza nguvu katika bechi la ufundi kuelekea mchezo huo wa ugenini.

 

“Kama ambavyo mnafahamu Zahera ni kocha mkubwa hivyo anaweza kuongeza jambo haswa kutokana na kuwa mzoefu na michuano mikubwa ya kimataifa, akiwa kama mkurugenzi wa maendeleo ya soka la vijana pia atakuwa na uwezo wa kutoa ushauri kwa benchi la ufundi lakini hata kuzungumza na wachezaji, hivyo tunaamini kazi hiyo itaanza ugenini huko Nigeria,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi lilimtafuta Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli ili aweze kuthibitisha habari hii lakini simu yake iliita na haikupokelewa.

 

Marco Mzumbe, Dar es Salaam

 

 

Leave A Reply