The House of Favourite Newspapers

Zahera Apewa Mtihani Yanga

KIKOSI cha Yanga jana asubuhi kilitua jijini Mwanza tayari kwa mechi zake mbili jijini humo katika Uwanja wa CCM Kirumba ambazo ni mtihani wa aina yake.

 

Mechi hizo ni ile ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC itakayochezwa Jumanne ijayo, lakini pia ile ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri itakayopigwa Oktoba 27.

 

Katika kuelekea mechi hizo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela ameliambia Spoti Xtra kuwa maandalizi yao kwa upande uongozi yamekamilika, kazi pekee iliyobakia ni benchi la ufundi la timu hiyo kuhakikisha wanapata ushindi.

 

Alisema kwa upande wa uongozi wamefanya kila kitu ikiwa ni pamoja na zawadi mbalimbali ambazo watawapatia wachezaji wao pindi watakapofanya vizuri katika mechi hizo.

 

Kwa upande wake kocha Mwinyi Zahera ameliambia gazeti hili kuwa; “Kila kitu nilichokuwa nimemwachia msaidizi wangu, Noel Mwandila wakati nilipokuwa katika majukumu ya timu ya taifa nimekuta kipo sawa.

 

“Kwa hiyo ni matumaini yetu kuwa tutafanya vizuri katika mechi hizo. Wachezaji wote wapo sawa isipokuwa Banka (Mohammed Issa) pamoja Issa Bigirimana ambao ni majeruhi na tutawakosa katika mechi hizo mbili,” alisema Zahera.

 

BOXER ANGALAU

Beki wa kulia ya Yanga, Paul Godfrey ‘Boxer’ sasa yupo tayari kwa kuiwakilisha timu hiyo katika mechi ya kimataifa dhidi ya Pyramids ya Misri. “Nipo fiti kwani mazoezi nilishaanza muda, nipo tayari kwa kuitumikia timu yangu kwa nguvu zangu zote kama ilivyokuwa zamani. “Hata ikitokea kocha akanipatia nafasi ya kucheza dhidi Waarabu nipo tayari,” alisema Boxer ambaye kwa sasa ni mmoja kati ya mabeki wa kulia wanaofanya vizuri hapa nchini.

Comments are closed.