The House of Favourite Newspapers

Zahera: Nakuja Jumapili, Tulieni

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo, amewatuliza mashabiki wa klabu hiyo ambao wanajua ameenda moja kwa moja kwa kuwaambia kwamba anarudi kuanza majukumu yake ya msimu ujao siku ya keshokutwa Jumapili.

 

Zahera amesema kuwa anatua ndani ya kikosi hicho na kuendelea na majukumu yake baada ya kumaliza siku zake za mapumziko ambayo alipewa ya siku 15 baada ya kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa lake DR Congo kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zilizofanyika Misri.

 

Awali ilikuwa ikitangazwa kuwa kocha huyo ameikacha Yanga na ndiyo maana akashindwa kujiunga na klabu hiyo ambayo imeweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika mkoani Morogoro.

 

Zahera ameliambia Championi Ijumaa, kuwa anatua Bongo kuja kuendelea na majukumu yake siku ya Jumapili ambayo Taifa Stars itakuwa inacheza na Kenya kwenye mechi ya Chan kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake baada ya muda wake wa mapumziko kumalizika tangu alipotoka Misri.

 

“Watu wamekuwa wakizungumza tu mambo mengi kwamba eti sitarudi Yanga, jambo ambalo halina ukweli wowote ule kwani mimi narudi wiki hii baada ya muda wangu wa mapumziko niliopewa baada ya kutoka kule Misri kwenye Afcon kumalizika.

 

“Nilipewa siku 15 na niliondoka Misri Julai 13, sasa ukipiga hesabu za siku 15 mbele utaona ni kwamba Julai 28 ndiyo natakiwa kurejea katika timu yangu kwa ajili ya kuendelea na programu za msimu ujao wa ligi na mashindano mengine,” alisema Zahera.

Comments are closed.