The House of Favourite Newspapers

Kumbe Pawa Benki si lolote!

0

Olixar_enCharge_Power_BankJUZIJUZI nilirudi kijijini kwetu kwenda kuwaona wazazi, na pia kushtaki kwani mambo kazini yalikuwa hayaendi sawasawa kabisa. Si unajua tena ukirudi kijijini kuna mambo mengi yanahusika.

Tena kama babu yako mzaa baba au mama yupo hai ukimwelezea matatizo yanayokukabili mjini, kama ni Wakristo watakuombea na kama ni Waislamu watafanya dua.

Pia kama ni wapagani watakufanyia mambo ya jadi au kukupeleka kwa mtaalam ili mjukuu wao uondokane na mikosi inayokufanya mambo yako yasikuendee vizuri, kisha watakwambia rudi mjini kila kitu kitakwenda sawa.

Basi siku ya kwanza unapofika kijijini ni salamu na kutembelea ndugu, japo unapewa masharti nani umtembelee na nani usikanyage kwake, hii inatokana na wanakijiji kujuana vizuri, kuwa kuna watu wengine ukiwasalimu tu na kama hujajitengeneza basi ndo ujue mikosi inakufuatia.

Siku ya tatu ndiyo ikawa ya kuanza shughuli za kujitengeneza, maana baada ya kuwaambia wazee kuwa mjini nafanya kazi lakini hela sijui inaenda wapi, ikakubalika lazima kuna mkono wa mtu.

Pia baada ya kulinganishwa na wenzangu ambao tulimaliza la saba wote, ikaonekana mimi tu ndiyo sina kitu, hata mke wala mtoto sina, ni wazi kulikuwa na kitu kinaziba nyota yangu.

Baada ya wazazi wangu ambao wanapenda sana mambo ya kishirikina kushauriana ni mtaalam yupi angefaa kuniwekea mambo yangu sawa, wakakubaliana wanipeleke kwa mmoja aliyekuwa anaishi kijiji cha jirani.

Basi  nikapelekwa kwa mtaalam huyo ambaye alipoangalia nyota ikagunduliwa kuwa kumbe pale kazini kwangu kuna jamaa wamechafua nyota yangu.

Hili liliniuma sana, mi mpiga debe stendi ya mabasi, washkaji wote nilijua rafiki zangu kumbe kuna wabaya wangu nacheka nao palepale kijiweni, dah roho iliniuma sana, nilimuomba mtaalam kama ikiwezekana mbaya wangu akutwe na mabaya zaidi, lakini mtaalam akasema hiyo siyo lazima, ila nikifika tu nitamjua mbaya wangu.

Basi mtaalam akanitengeneza, kisawasawa, chale mwili mzima, akanipa na hirizi kubwa, siku hizi watoto wa mjini wanaiita Pawa Benki, nikaruhusiwa kurudi kazini.

Baba akalipa mbuzi mweusi mwenye doa jeupe nikaruhusiwa kurudi mjini. Kiukweli wakati narudi furaha ilikuwa imenijaa moyoni, maana niliambiwa mbaya wangu nitamjua na atakayenijaribu kila kitu kitamrudia mwenyewe.

Leo nimemaliza mwezi, mbaya wangu sijamjua, na hela ngumu kama mwanzo. Nafikiria kurudi kijijini tukanyang’anye yule mbuzi nimuuze, japo nipate hela ya siku mbili tatu.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply