The House of Favourite Newspapers

Mchungaji Mbaroni kwa Kuwanywesha ‘Sumu’ Waumini

0

MCHUNGAJI Sam Little (25) ambaye ni raia wa Uingereza amekamatwa nchini Uganda kwa tuhuma za kuwanywesha waumini wake dawa ya kujichubua na kuwaaminisha kuwa ni tiba ya miujiza inayotibu magonjwa ya malaria, saratani (kansa) na Ukimwi.

 

Mchungaji huyo wa Kanisa la Global Healing Christian Missions alikamatwa hivi karibuni baada ya gazeti la Guardian la Uingereza kufi chua mtandao wa uovu huo na kuainisha namna Little alivyokuwa anashirikiana na mchungaji mwingine Robert Baldwin kutoka Marekani kusambaza dawa hiyo iliyopewa jina la ‘mchanganyiko wa madini wenye miujiza’ kwa kifupi MMS.

 

Sam Little ambaye anatokea katika mji wa Bedfordshire nchini Uingereza, alikamatwa na askari wa Uganda katika makazi ya Kanisa lake lililopo katika kijiji cha Kitembi, maili chache kutoka mji wa Fort Portal uliopo magharibi mwa Uganda.

 

 

Mbali na mchungaji huyo pia walikamatwa raia wawili wa Uganda ambao walikuwa wakishirikana naye kutoa huduma ya kuwanywesha Waganda dawa hiyo ambayo tangu mwaka 2010 ilikwishapigwa marufuku na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa kuwa ni sumu.

 

 

Hadi watuhumiwa hao watatu wanakamatwa, tayari imeelezwa kuwa zaidi ya raia 50,000 wa Uganda walikuwa wamenyweshwa dawa hiyo wakiwamo watoto wadogo kwa imani kuwa watapona magonjwa yao.

 

 

Kuibuka kwa ripoti hiyo ya Guardian, kulisababisha Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Uganda, kutoa onyo kwa vyombo vya dola nchini Uganda, Kumchukulia hatua mchungaji huyo kwa kusambaza dawa hiyo ambayo ilikuwa ikisambazwa nchini humo kwa ufadhili wa mchungaji huyo wa Marekani licha ya kimiminika hicho kudhibitishwa kuwa hakitibu magonjwa yoyote zaidi ya kusababisha madhara katika mwili wa binadamu.

 

 

Taarifa zilidai kuwa Robert Baldwin, alikuwa akiingiza kontena za mchanganyiko wa madini ya Chloride dioxide kutoka China, na kuwafundisha Waganda zaidi ya 1200 namna ya kuyachanganya kabla ya kuyasambaza kwa waumini kama miujiza ya kujitibia magonjwa.

 

 

Mchungaji huyo Baldwin alikuwa akitoa simu rununu ‘smartphone’ kwa wachungaji ambao walikuwa wamejitolea kusambaza tiba hiyo ya miujiza kwa washirika wao.

 

 

Aidha, polisi nchini Uganda walitoa wito kwa umma hususani jumuiya ya wakristo ambao ni zaidi ya asilimia 85 nchini humo kuwa makini na miujiza ya uongo. Pia walisema tayari sampo za kimiminika cha madini hayo kimepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Leave A Reply