The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness – 62

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi.
Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya bila mtu yeyote kujua kwamba bado yupo hai, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake. Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Haikuwa rahisi kwa familia ya Njoroge ambayo ndiyo iliyomlea Brianna kukubaliana na kilichokuwa kinazungumzwa na Diego lakini alipoingizia suala la kiwango cha fedha ambacho wangekipata, ukichanganya na maisha ya dhiki waliyokuwa wanaishi, Njoroge na mkewe walijikuta wakibaki njia panda.
“Kwa hiyo wewe ulikuwa unasemaje baba?”
“Kama tumekubaliana, nampigia simu Msuya na kumwambia tumempata Arianna, mambo mengine yote niachieni mimi.”
“Na wewe Brianna unasemaje?”
“Nikikubali kwenda nitaenda kuendelea na masomo ya sekondari? Halafu siku akigundua kwamba mimi siyo huyo aliyekuwa anamtaka itakuwaje?”
“Msuya ni mtu mmoja mzuri sana, atakusomesha hata ukitaka mpaka chuo kikuu. Isitoshe hawezi kugundua chochote kwa sababu hakuna tofauti kati yako na Arianna hata kidogo, mmefanana sana na mambo mengine nitakuwa nakufundisha taratibu.”
“Basi nipo tayari ila sitakuwa tayari kushiriki naye tendo la ndoa.”
“Usijali kuhusu hilo, uamuzi ni wako,” alisema Diego huku akionesha kufurahishwa mno na jinsi msichana huyo alivyokuwa mwelewa.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka Diego alichukua simu yake na kumpigia Msuya na muda mfupi baadaye alipokea.

“Kuna taarifa njema huku, Arianna amepatikana Mathare, Nairobi na hivi tunavyozungumza nipo naye lakini inaonesha kama mambo yaliyotokea yamemuathiri kisaikolojia, anakuwa kama mtu aliyepoteza kumbukumbu na wakati mwingine anaongea mambo yasiyoeleweka,” alisema Diego, kauli iliyomfanya Msuya apige kelele na kurukaruka kwa furaha kubwa.
Hakuna kitu alichokuwa anakisubiri kwa hamu kama taarifa za kwamba Arianna alikuwa hai, hakutaka kujali kitu kingine chochote, akawa anamshukuru Mungu wake kwa muujiza mkubwa aliomtendea. Ilibidi Diego akate simu kwanza kwa sababu  hakukuwa na hali ya kusikilizana tena kati yake na Msuya kutokana na furaha aliyokuwa nayo.
Muda mfupi baadaye, Msuya alipiga tena simu, akamtaka Diego amhakikishie kama ni kweli, akampa majibu yaleyale na kumwambia kama alikuwa haamini, azungumze na watu waliofanikisha kupatikana kwake.

Akampa simu mzee Njoroge ambaye alimhakikishia kwamba yeye ndiye aliyefanikisha kupatikana kwa msichana huyo, akazidi kufurahi na kuahidi kwamba muda mfupi baadaye atakuwa ameshafika jijini Nairobi.
Hakutaka kupoteza muda, aliwasiliana na rafiki yake aliyemkodishia helikopta jana yake ambapo alikubali kumpa tena. Dakika arobaini baadaye, tayari Msuya alikuwa ndani ya helikopta, akiwa na kiwango cha fedha alichoahidi kukitoa kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa Arianna.
Baada ya kusafiri kwa muda mrefu angani, hatimaye waliwasili jijini Nairobi, rubani akatafuta sehemu nzuri ya kutua kisha Msuya akashuka na kukodi teksi iliyompeleka mpaka Mathare huku muda wote akiwasiliana na Diego ambaye alimuelekeza mpaka nyumbani kwa mzee Njoroge.

Msuya hakuamini macho yake alipofika nyumbani hapo na kumkuta Brianna ambaye yeye aliamini ni Arianna, akiwa amekaa kwenye mkeka huku mzee Njoroge, mkewe na Diego wakiwa wamekaa pembeni.
“Arianna! Ni wewe? Siamini mke wangu,” alisema Msuya kwa sauti kubwa, machozi yakawa yanambubujika na kuulowanisha uso wake, akapiga magoti pale chini msichana huyo alipokuwa amekaa na kumkumbatia kwa nguvu.
Brianna alibaki amepigwa na butwaa, kwanza hakutegemea huyo Msuya aliyekuwa akiambiwa alikuwa mtu mzima kiasi kile na pili hakutegemea alikuwa na ukaribu na mkewe kiasi hicho kwa sababu alimkumbatia kwa nguvu na kumbusu, hali iliyoonesha alikuwa akimpenda sana.

“Uko sawa? Hawajakuumiza au kukudhuru kwa chochote? Vipi mwanangu?” Msuya alisema huku akimuachia msichana huyo na kuanza kumkagua sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni. Brianna alishindwa kujibu chochote zaidi ya kuwa anatingisha kichwa kuonesha kwamba yuko sawa.
Ilibidi Diego amvute Msuya pembeni kwani kama angeendelea kumdadisi zaidi, huenda angeshtukia kwamba hakuwa Arianna. Akamwambia kwamba kutokana na matukio aliyopitia, wameshauriwa kwamba apewe muda mwingi wa kupumzika ili akili itulie kwa sababu bado hakuwa sawa, Msuya akawa anatingisha kichwa huku akigeuka na kumtazama msichana huyo kwani na yeye aligundua kwamba hakuwa sawa.
“Kwa hiyo nini cha kufanya hapa?”
“Mimi nafikiri tuwakabidhi hawa watu waliofanikisha kupatikana kwake zawadi yao kisha tuondoke naye kurudi nyumbani, bado hali ya kiusalama si shwari huku,” alisema Diego, wazo ambalo Msuya alilikubali haraka.
Njoroge na mkewe wakakabidhiwa kitita cha shilingi milioni mbili na laki tatu za Kenya, sawa na takribani shilingi milioni hamsini za Tanzania, kiwango ambacho ndicho kilichoahidiwa kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa msichana huyo.

Kwa mzee Njoroge na mkewe, huo ulikuwa ni zaidi ya muujiza kwao, hawakuwahi kuwaza hata siku moja kwamba watakuja kushika kiwango kikubwa cha pesa namna hiyo. Wakawa wanamshukuru Mungu wao kwa muujiza huo.
Baada ya makabidhiano hayo, hakukuwa na muda wa kupoteza, Msuya, Diego na msichana huyo waliondoka kwa usafiri aliokuja nao Msuya mpaka sehemu alikoiacha helikopta iliyomleta kutoka Tanzania.
Muda wote Brianna alikuwa amejiinamia, machozi yakimtoka kwani alijisikia vibaya sana kutenganishwa na familia ya Njoroge ambayo kwake ndiyo walikuwa ndugu pekee aliokuwa anawafahamu.
Hatimaye walipanda kwenye helikopta na muda mfupi baadaye, safari ya kurejea Tanzania ilianza huku muda wote Msuya akiwa amemshika begani Brianna, akawa anazungumza maneno ya kumshukuru Mungu wake kwa kumlinda msichana huyo mpaka muda huo.

Baada ya safari ndefu na ngumu, huku mara kwa mara helikopta waliyokuwa wakisafiria ikinusurika kupata ajali kutokana na hali mbaya ya hewa, hatimaye waliwasili jijini Arusha na kwenda moja kwa moja mpaka jirani na nyumbani kwa Msuya ambapo ilitua kisha wote wakateremka.
Kila kitu kilikuwa kigeni kwa Brianna, akawa anashangaa pale ni wapi maana hakuwahi kufika hata mara moja. Kila macho yake yalipokuwa yakigongana na ya Diego, alikuwa akimpa ishara ya kutulia kwani kama angeendelea hivyo, msuya angeweza kushtuka.

Kitendo cha kuingia tu ndani ya nyumba hiyo, ndugu, jamaa na marafiki wengi wa Msuya ambao walikuwa wamekusanyika nyumbani hapo kwa ajili ya kusaidiana kumtafuta Arianna, walimkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu huku wakiwa hawaamini kama amerejea salama.

Kwa Brianna kila kitu kilikuwa kigeni, akawa anamshangaa kila mtu mpaka watoto wa Msuya pamoja na wafanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo. Ilibidi Msuya awawahi watu wote na kuwaeleza kwamba kutokana na matukio yaliyompata Arianna, akili yake haikuwa imetulia hivyo anahitaji muda wa kupumzika, jambo ambalo kila mtu alilielewa.

Furaha kubwa ikatanda kwenye nyumba hiyo, klila mtu akawa anamshukuru Mungu wake kwa kilichotokea. Msuya na Diego walipitiliza hadi ndani wakiwa na msichana huyo na kumpeleka sebuleni ambapo hakukaa sana, Msuya akamtaka waelekee chumbani.
Brianna alishindwa kubisha, mwanaume huyo akamshika mkono na kumuongoza kupanda kwenye ngazi za kuelekea chumbani na muda mfupi baadaye, tayari walikuwa chumbani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply