The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 078

1

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.
Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.
Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.
Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.
Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.
Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Cha ajabu, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, Jafet anapowasili nchini India, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Anna anakuwa gumzo kila sehemu.
Baada ya afya yake kuimarika, anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo. Anaongozana na wazazi wake mpaka hotelini na mipango ya kurejea nyumbani Tanzania inaanza na tayari wapo uwanja wa ndege.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kukamilisha taratibu zote uwanjani hapo, wote wanne waliingia mpaka ndani kabisa na kwenda kwenye ndege kubwa ya Fly Emirates waliyopanga kuondoka nayo. Wakaungana na abiria wengine kupanda kwenye ngazi za ndege hiyo na muda mfupi baadaye, kila mmoja alikuwa amekaa kwenye siti yake, Anna akiwa amekaa siti moja na Jafet. Safari ya kurejea Tanzania ikaanza.
Baada ya kusafiri kwa saa nyingi angani, hatimaye sauti ya mhudumu wa kike wa ndege ilisikika ikiwataarifu abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Jafet alimtingisha Anna aliyekuwa amelala fofofo kwenye kifua chake, akamsaidia kufunga mkanda kwenye siti yake na kuendelea kumuamsha.
“Wake up Anna, we are already at home, wake up,” (Amka Anna, tayari tumeshafika nyumbani, amka) alisema Jafet huku akiendelea kumtingisha Anna. Msichana huyo alizinduka kutoka usingizini na kuanza kuangaza macho nje kupitia kwenye kioo cha pembeni ya siti aliyokuwa amekaa.
“Whaoo! Thanks God we are back home safely,” (Whaoo! Ahsante Mungu tumerudi salama nyumbani) alisema Anna huku akijinyoosha pale alipokuwa amekaa. Muda mfupi baadaye, ndege ilianza kuinama upande wa mbele kuonesha kwamba ilikuwa ikienda kutua.
Ikashuka kwa kasi na muda mfupi baadaye, magurudumu yake yaligusa ardhi na kusababisha itingishike kidogo kisha ikarudi kwenye hali yake ya kawaida, ikaendelea kukimbia kwa kasi na dakika kadhaa baadaye, ilisimama pembeni ya jengo kubwa la uwanja huo wa ndege.
Magari maalum yaliyokuwa na ngazi yaliisogelea ndege hiyo kisha milango ilifunguliwa na abiria wakaanza kushuka, mmoja baada ya mwingine. Jafet, Anna na wazazi wa msichana huyo walikuwa miongoni mwa abiria walioteremka kwenye ndege hiyo.
Wakaenda mpaka ndani ya jengo hilo la uwanja wa ndege na kusubiri mizigo yao. Hata hivyo, kwa kuwa bado walikuwa na safari ya kuelekea jijini Mwanza, walitaka kuunganisha ndege lakini Anna alionesha kuwa mgumu kukubaliana na suala hilo.
“Kwa nini tusipumzike kidogo hapa Dar es Salaam halafu kesho ndiyo tukaendelea na safari?”
“Hapana Anna, tumekaa siku nyingi nje ya nchi, mambo mengi yamesimama nyumbani, inabidi tufike leoleo. Isitoshe inatakiwa tufike mpaka kijijini kwa akina Jafet kuwashukuru wazazi wake na kuwakabidhi mtoto wao,” alisema baba yake Anna lakini msichana huyo akawa mbishi.
“Kama nyie mna haraka tangulieni sisi tutakuja kesho na Jafet,” alisema Anna kwa sauti ya kudeka, jambo lililosababisha wazazi wake wavutane pembeni na kuanza kujadiliana.
“Hakuna haja ya kuwahi, tukubaliane tu na Anna, tutafute hoteli nzuri tukampumzike halafu kesho tutaendelea na safari, mi mwenyewe najihisi kuchoka sana,” alisema mama yake Anna, kauli iliyomfanya mzee huyo akose majibu. Wakakamilisha taratibu zote uwanjani hapo kisha wakaungana na abiria wengine na kutoka kupitia lango kuwa lililokuwa na maandishi juu yaliyosomeka ‘Arrivals/ Wanaowasili’.
“Najisikia raha sana kurejea nyumbani Tanzania, tena nikiwa na afya imara kabisa,” alisema Anna huku akikimbiakimbia kwa furaha wakati wakielekea kwenye maegesho ya teksi. Muda mfupi baadaye, tayari walikuwa ndani ya teksi, baba yake Anna akakaa siti ya mbele, nyuma wakakaa Anna, mama yake na Jafet.
“Tupeleke Del Monte Hotel,” alisema baba yake Anna na muda mfupi baadaye safari ikaanza. Anna akawa anaendelea kufurahi huku mara kwa mara akimlalia Jafet kifuani na kumbusu. Hakujali kwamba wazazi wake walikuwepo, mapenzi yake kwa Jafet yalikuwa yamerudi kwa kasi kubwa, kuliko hata ilivyokuwa mwanzo.
Alimuona kijana huyo mpole, mstaarabu, muungwana na mwenye mvuto kuwa kama mungu wake kwani bila yeye, afya yake isingeimarika kiasi hicho. Hatimaye waliwasili Del Monte Hotel, baba yake Anna akamlipa dereva teksi huyo kisha wakasaidiana kuteremsha mizigo yao na kupokelewa na wahudumu wachangamfu wa hoteli hiyo.
Wakakaribishwa mpaka ndani ambapo baba yake Anna alilipia vyumba vitatu, kimoja kwa ajili yake na mkewe, kingine kwa ajili ya Jafet na kingine kwa ajili ya Anna.
“Sasa baba huoni kama unatumia vibaya pesa? Kwa nini mimi na Jafet tusilale chumba kimoja kama jana tukiwa India?”
“Hapana Anna, kila mtu inabidi alale kwenye chumba chake,” alisema baba yake Anna akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara, ikabidi Anna atulie na kutii baba yake alichokuwa anakisema. Hata hivyo, moyoni mwake alijiapiza kuwa lazima siku hiyo akamilishe jambo alilokuwa akilisubiri kwa kipindi kirefu.
“Jafet! Umelala?” Anna aliuliza kwa sauti ya chini baada ya kunyata na kutoka chumbani kwake na kuelekea kwenye chumba cha Jafet.
“Bado sijalala, vipi mbona unaingia kama mwizi?”
“Sitaki baba ajue kwamba nimekuja huku si umemsikia ameanza kuchonga,” alisema Anna na kusogea mpaka kitandani ambapo Jafet alikuwa amejilaza, akiwa amejifunga taulo tu baada ya kutoka kuoga muda mfupi uliopita.
“Jafet! Nakupenda sana mwenzio na leo naomba unifurahishe moyo wangu, naomba unipe haki yangu,” alisema Anna na kuanza kuvua blauzi aliyokuwa ameivaa, akaitupa pembeni na kuhamia kwenye suruali, nayo akaivua na kuitupa.
“Hapana Anna! Noo,” alisema Jafet baada ya kumuona msichana huyo akimalizia kuvua nguo zilizokuwa zimesalia lakini tayari alikuwa amechelewa. Anna akiwa kama alivyoletwa duniani, alimvamia Jafet pale kitandani huku akionesha kudhamiria kutimiza azma yake.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment
  1. nnicraus says

    Jafet hapo unalo maan hyo mtto ni shiiidaa kam vp maliz den kuw mpole

Leave A Reply